Habari

KAMATI YA BUNGE YAIDHINISHA MPANGO WA MATUMIZI WA WIZARA YA ARDHI 2026/2027

  • 31 Mar, 2026
KAMATI YA BUNGE YAIDHINISHA MPANGO WA MATUMIZI WA WIZARA YA ARDHI 2026/2027

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhia Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2026/2027. 

 

Uamuzi huo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Timotheo Mzava unafuatia kikao cha uwasilishaji wa Randama kwa mwaka 2026/2027 uliofanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Kamati hiyo tarehe 30 Machi 2026 Bungeni jijini Dodoma.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kuridhia mpango huo wa matumizi wa Wizara yake kwa mwaka 2026/2027 na kusisitiza kuwa wizara hiyo itazingatia na kutekeleza maelekezo yote ya kamati katika mpango huo ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na tija.

 

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya, Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga, Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy Kabyemera, Wajumbe wa Menejimenti, wataalam Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini Wizara hiyo.