Habari
KABYEMERA: MPANGO WA UENDELEZAJI SINZA HAULENGI KUTWAA ARDHI YA WANANCHI
- 10 Aug, 2026
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera amesema kuwa, Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Sinza katika manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam haulengi kutwaa ardhi ya wananchi.
Bi. Kabyemera ametoa kauli hiyo mapema leo Agosti 9, 2026, wakati akitoa elimu kuhusu uendelezaji eneo hilo kwa wamiliki wa nyumba na ardhi wa Sinza katika Ukumbi wa Mawela, Sinza, Dar es Salaam.
“Mpango huu haulengi kuchukua wala kutwaa Ardhi ya mtu anayemiliki kwa taratibu na kwa mujibu wa sheria, bali unalenga kuhuisha matumizi ya ardhi, kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa huduma na kuongeza thamani ya ardhi,” amesema
Amefafanua kuwa, Serikali inaendelea kutekeleza mpango huo kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria zote, huku ikihakikisha hakuna hatua itakayokiuka haki za mtu anayemiliki ardhi kihalali.
Akizungumzia sheria na miongozo inayosimamia mpango huo, amesema yote inalenga kumpatia mwananchi makazi bora, pamoja na kusimamia maendeleo ya makazi na miji kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo.
Kwa mujibu wa Bi. Kabyemera, mpango wa kuendeleza Sinza si matakwa ya Serikali pekee, bali unazingatia pia mapendekezo na mahitaji ya wananchi, huku mkutano huo ukiwa ni fursa ya kuwaeleza wananchi haki na maslahi yao katika utekelezaji wa mpango huo.
Aidha, amewataka wananchi kupuuza taarifa zinazodai kuwa kuna mwekezaji anayekuja kuchukua eneo la Sinza, akisisitiza kuwa kinachofanyika ni kuboresha eneo hilo, kukidhi mahitaji ya sasa na kuzuia uendelezaji holela wa mji.
Amewashukuru wananchi wa Sinza kwa ushirikiano wanaouonesha kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa mafanikio na kuleta matokeo chanya utakapo kamilika.
Aidha, amewataka wananchi hao wa Sinza kutumia vyema fursa ya mikutano hiyo kwa kutoa maoni na kuuliza maswali, ili pamoja na Serikali kujenga uelewa wa pamoja, jamii isije ikapotoshwa kuhusu malengo halisi ya Mpango wa Uendelezaji Upya wa Sinza.