Habari

JERRY SILAA AYATAKA MABARAZA YA ARDHI YA KATA KUZINGATIA MABADILIKO YA SHERIA USULUHISHI WA MIGOGORO YA ARDHI

  • 13 Oct, 2023
JERRY SILAA AYATAKA MABARAZA YA ARDHI YA KATA KUZINGATIA MABADILIKO YA SHERIA USULUHISHI WA MIGOGORO YA ARDHI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Slaa ameyataka Mabaraza ya Ardhi ya Kata kuzingatia mabadiliko ya Sheria namba tatu ya mwaka 2021 inayoyataka Mabaraza hayo kufanya kazi ya usuluhishi kwa kipindi kisichozidi siku 30 na si vinginevyo.

Aidha Waziri Silaa amewataka wananchi kutambua kuwa Mabaraza ya Kata hayawajibiki katika kujihusisha na migogoro ya ndoa, madai au jinai bali kazi yake ni usuluhishi wa migogoro ya ardhi ndio maana yakaitwa Mabaraza ya Ardhi ya Kata.

''Ikiwa Baraza la Kata limefanya usuluhishi wa mipaka kati ya jilani na jilani au usuluhishi wa mauzo kwa kipindi cha siku 30 endapo makubaliano ya pande mbili hayakufikia maridhiano wanapaswa kuwapa nyaraka pande zinazosigana kwenda Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ambalo liko chini ya Wizara Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.''Aliongeza Jerry Silaa Waziri wa Ardhi.

Waziri Silaa pia ametoa wito kwa wananchi wote wenye malalamko ya kiutendaji yatokanayo na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kuwasilisha malalamiko yao kwa maandishi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi kwani watendaji wa Mabaraza hayo wanawajibika kwake  moja kwa moja.

''Kama mwananchi hajaridhika na maamuzi ya Kisheria yanayotolewa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya basi afuate utaratibu wa kawaida wa kukata rufaa kwenda Mahaka Kuu lakini kama ana malalamiko ya kiutendaji na nidhamu basi malalamiko hayo yaletwe na kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi ili tuyafanyie kazi.'' ''Aliongeza Jerry Silaa Waziri wa Ardhi.

Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yana mamlaka ya kusikiliza  na kuamua migogoro ya ardhi yeye thamani isiyozidi milioni mia 200 kwa mali inayohamishika na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. Milioni mia 300 za kitanzania.

Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya yanaanzishwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Sura 2016 namba 2 ya Mwaka 2002.

Kwa upande wa Mabaraza ya Kata Sheria ya Mabaraza ya Kata Sura 206 na Sheria ya Mahakama ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Sura 216 Waziri wa TAMISEMI ndiye mwenye Mamlaka ya Kusimamia Mabaraza ya Kata na kwa niaba yake jukumu hilo linatekelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri.