Habari

FURAHA ZATANDA MLANDIZI, MGOGORO WA ARDHI WA MIAKA 20 NGETA UKITATULIWA, WANANCHI WAANZA ENZI MPYA YA MAENDELEO

  • 11 Aug, 2026
FURAHA ZATANDA MLANDIZI, MGOGORO WA ARDHI WA MIAKA 20 NGETA UKITATULIWA, WANANCHI WAANZA ENZI MPYA YA MAENDELEO

Wananchi wa Kitongoji cha Makazi Mapya, Kata ya Kawawa wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanikisha utatuzi wa mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kati ya wakazi wa Makazi Mapya na Kitongoji cha Ngeta.

 

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa njia ya haki, mazungumzo na ushirikishwaji wa jamii.

 

Akizungumza katika mahojiano maalumu, Diwani wa Kata ya Kawawa, Mhe. Alfred Daniel Malega, amesema utatuzi wa Mgogoro huo umeondoa hofu na migawanyiko iliyokuwepo kwa muda mrefu, na sasa wananchi wameanza ukurasa mpya wa amani na maendeleo.

 

"Mgogoro huu ulidumu kwa zaidi ya miaka 20 na ulikuwa ukikwamisha maendeleo ya wananchi. Leo tunaishukuru Wizara ya Ardhi kwa kutuletea suluhisho la kudumu. Sasa tuna amani na tunaelekeza nguvu zetu katika maendeleo,” amesema.

 

Mhe. Malega meongeza kuwa, eneo lenye ukubwa wa hekta 93.5, lililotengwa kwa ajili ya huduma za kijamii, sasa litatumika kwa ujenzi wa shule ya sekondari na zahanati pamoja na  miradi itakayonufaisha maelfu ya wakazi wa eneo hilo.

 

Kwa nyuso zenye tabasamu na sauti za shukrani, wananchi wa Makazi Mapya na Ngeta Bi.Agatha Petro Kibage,Bw.Elly Elia Mtandi na Bi.Nuru Said Matimbwa wamesema utatuzi wa mgogoro huo umeondoa tofauti alizozieleza kuwa zimekuwa zikivuruga mshikamano wa jamii, na kwamba sasa wanaishi kama ndugu wenye lengo moja la kuijenga Mlandizi.

 

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makazi Mapya, Bw. Saidi Kilindi, pamoja na Katibu wa Serikali ya Kitongoji, Bw. Adriano Kassimu Gama, wameipongeza Serikali na Wizara ya Ardhi kwa kusimamia mchakato wa upatanisho hadi kufikia tamko la mwisho lililotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo.

 

Wamesema, tamko hilo limeweka bayana kuwa mgogoro kati ya Makazi Mapya na Ngeta umehitimishwa rasmi, huku kila upande ukiendelea kuheshimu mipaka na mahusiano ya kijamii bila uhasama.  

 

Utatuzi wa mgogoro huo unaendelea kuonesha namna Serikali inavyoweka mbele maslahi ya wananchi kwa kulinda haki za umiliki wa ardhi, kuimarisha amani na kufungua fursa za maendeleo endelevu katika jamii.

 

Hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilitoa msimamo wa kufunga shauri la mgogoro wa ardhi uliohususu baadhi ya wananchi wa Ngeta, Kata ya Kikongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani baada ya kubainika kuwa madai ya walalamikaji hayakuwa na msingi wa kuendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

 

Wananchi hao wanadai kuwa walihamishwa kutoka katika maeneo yao wakati wa Operesheni Vijiji na kuacha mashamba pamoja na mazao ya kudumu, yakiwemo ya mikorosho, lakini baadaye maeneo hayo yakamilikishwa kwa watu wengine bila wao kulipwa fidia.