Habari

E-ARDHI YAFANYA KAZI: VIWANJA 4,851 VYAPANDISHWA NA KUHIDIHINISHWA TABORA NA KIGOMA

  • 17 Sep, 2026
E-ARDHI YAFANYA KAZI: VIWANJA 4,851 VYAPANDISHWA NA KUHIDIHINISHWA TABORA NA KIGOMA

Utekelezaji wa Mfumo wa e-Ardhi katika Mikoa ya Tabora na Kigoma umeonesha mafanikio makubwa katika kuongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa huduma za ardhi.

 

Akizungumzimzia utekelezaji wa zoezi hilo Mjumbe wa Timu ya usambazaji wa Mfumo kutoka Wizara ya Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw.Makwasa Msase Biswalo amesema Katika kipindi cha siku sita, Mkoa wa Tabora umefanikiwa kupandisha na kuidhinisha viwanja 3,291, huku Hati 66 zikitolewa kupitia Manispaa ya Tabora na Halmashauri ya Mji wa Nzega.

 

Amesema,Kwa upande wa Kigoma, viwanja 1,560 vimepandishwa na kuidhinishwa, huku Hati 19 zikitolewa kwa wananchi kupitia mfumo huo.

 

 Bw.Biswalo amesema matokeo hayo yanaonesha mwitikio mzuri wa watumishi katika matumizi ya mfumo.

 

Hata hivyo, baadhi ya Hati Kigoma bado hazijachapishwa kutokana na kutokuwepo kwa pad za saini za wananchi, zinazohitajika kukamilisha mchakato wa uchapishaji.

 

Naye Kaimu Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kigoma, Bw. Tumaini Gwakisa, amesema mwitikio wa watumishi katika mafunzo na matumizi ya mfumo huo umekuwa mkubwa na umechangia mafanikio hayo.

 

Mafanikio hayo yanaonesha hatua ya Serikali katika kutumia teknolojia kuboresha usimamizi wa ardhi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa haraka, ufanisi na uwazi.