Habari
e- ARDHI KUSAIDIA WATENDAJI SEKTA YA ARDHI LINDI KUTOA HUDUMA KWA HARAKA
- 17 Sep, 2026
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendela na mafunzo ya siku nane ya mfumo mpya wa kidijiti wa e-Ardhi mkoani Lindi huku mfumo huo ukielezwa kusaidia watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo kutoa huduma kwa haraka pamoja na kupunguza urasimu kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Sept 16, 2026 mkoani Lindi Afisa Ardhi Mteule wa Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Kilwa Bw. Andrew Munisi amesema, mfumo huo utasaidia utoaji huduma kwa haraka ikiwemo wananchi kupata hati zao ndani ya siku moja au mbili, kulingana na maagizo ya Waziri wa Ardhi ya hati kutolewa ndani ya saa 48 kwa waliokamilisha taratibu za umiliki.
"Tunafurahi sana kupokea haya mafunzo ya mfumo mpya wa e-Ardhi katika mkoa wetu wa Lindi kwa sababu utasaidia makundi mbalimbali sambamba na kuondoa urasimu wakati wa kupata huduma na zile fursa za rushwa". Amesema
Akielezea faida ya mfumo huo kwa wananchi, Bw. Munisi amesema mfumo huo wa e-ardhi utapunguza muda wa wananchi kwenda kufanya maombi ofisini sambamba na ule msongamano wa kupata huduma.
Kwa upande wake, Salome mabula , ambaye ni Afisa Mipango Miji wa manispaa ya lindi ameuelezea mfumo wa e-ardhi kwamba utawasaidia wao kama watendaji wa sekta ya ardhi katika mawasiliono kutoka Idara moja kwenda nyingene kwa kuwa kila taarifa ya mteja itakua inaoneka kupitia mfumo na kujulikana kwa haraka hatua iliyopo.
Naye Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Ardhi, Makao Makuu Dodoma, Bw. Haruna Issa, amesema mwananchi yeyote mwenye 'intaneti' anaweza kupata huduma kwa kuingia kwenye tovuti ya ardhi (lands.go.tz) kwa kutumia namba yake ya NIDA na namba ya simu.
"Mfumo huu katika mkoa wetu hapa Lindi ni mpya na utamfanya mwananchi kuweza kuomba huduma yoyote hata akiwa nyumbani kwake sio lazima aje ofisini," alisema Bw. Haruna
Kwa mujibu wa Afisa huyo TEHAMA wa Wizara ya Ardhi, mfumo huo pia unamuwezesha mwananchi kujikadiria kodi ya pango la ardhi, kupata namba ya malipo (control number) na kulipia moja kwa moja pamoja na kufuatilia hatua ya maombi kuanzia mwanzo hadi kukamilika.
Utekelezaji mfumo wa e-Ardhi umeelezwa kuwa, ni moja ya hatua kubwa katika sekta ya ardhi nchini kwa kuwa unatarajiwa kuondoa kero za kupotea majalada ya karatasi, kuongeza makusanyo ya serikali, na kuharakisha utoaji hati na nyaraka za kisheria za ardhi kwa wananchi.