Habari

DKT BITEKO AZINDUA KITUO CHA TAIFA CHA UBUNIFU NA MAFUNZO YA TAAARIFA ZA KIJIOGRAFIA

  • 12 Sep, 2023
DKT BITEKO AZINDUA KITUO CHA TAIFA CHA UBUNIFU NA MAFUNZO YA TAAARIFA ZA KIJIOGRAFIA

Na Munir Shemweta, WANMM

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Doto Biteko amezindua kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya taarifa za kijiografia na kuitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kujitathmini katika utekelezaji majukumu yake ya msingi badala ya kuwa wizara ya inayoshughulika na utatuzi wa migogoro.

Dkt Biteko amesema hayo tarehe 9 Septemba, 2023 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuzindua kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya taarifa za kijiografia kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa.

"Kazi kubwa ya Wizara hii ni kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, sasa tujipime na tujitathmini kama katika sekta yetu ya ardhi kazi hizi tunazifanya kwa ukamilifu wake'' alisema.

Aidha, ameitaka Wizara hiyo kushirikiana na Halmashauri zote nchini ili kazi zifanyike kwa ushirikiano na kuondoa urasimu pamoja na migogoro ya ardhi.

Akigeukia kituo alichokizindua, Naibu Waziri huyo Mkuu na Waziri wa Nishati alisema, kituo hicho muendelezo wa hatua zinazochukuliwa na Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuchochea matumizi ya teknolojia sambamba na kuhakikisha ardhi inapangwa, inapimwa na kumilikishwa.

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa alisema, kituo kilichozinduliwa mbali na kusaidia kutoa ujuzi kwa watumishi kitawezesha pia kupunguza gharama sambamba na upimaji eneo kubwa kwa muda mfupi.

Alikielezea kituo hicho kuwa, ni muhimu kwa kuwa pamoja na mambo mengine kitaboresha shughuli za upimaji ardhi, uandaaji ramani za msingi, ujenzi wa miundombinu na kupanga matumizi bora ardhi.

Hafla ya uzinduzi wa kituo hicho ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii.