Habari
DKT AKWILAPO: WIZARA YA ARDHI IKO TAYARI KUSHIRIKIANA KUTAYARISHA RAMANI YA UWANJA WA NYAKABINDI- BARIADI
- 10 Aug, 2026
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Wizara yake ipo tayari kushirikiana na mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki pamoja na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuandaa ramani ya uwanja ikiwemo mpangilio kulingana na mahitaji ya eneo la Viwanja vya Maonesho Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.
Mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki katika maonesho ya Wakulima (Nanenane) ni mkoa wa Simiyu, Mara pamoja na Shinyanga.
Dkt. Akwilapo amesema hayo Agosti 8, 2026 wakati akifunga Maonesho na Sherehe za Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Mashariki, yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.
Amesema, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itasaidia kutoa muongozo wa umiliki wa eneo la uwanja na kuandaa mpango endelevu wa matumizi yake.
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, upangaji mzuri wa eneo ni msingi muhimu katika kuhakikisha shughuli na miundombinu inayotekelezwa katika viwanja hivyo inakuwa ya kudumu, inatumika kwa ufanisi na inaepusha migongano ya matumizi ya ardhi hapo baadaye.
“Wizara yetu ipo tayari kushirikiana na mikoa inayounda Kanda ya Ziwa Mashariki, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutayarisha ramani na mpangilio wa matumizi ya eneo hili kulingana na mahitaji yaliyopo na yajayo” amesema Dkt. Akwilapo.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha amesema maonesho na sherehe za wakulima (Nanenane) katika mkoa wake yalilenga kutoa fursa kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujenga ushirikiano na kutangaza bidhaa wanazozalisha katika maeneo yao.
Amewashukuru washiriki wa maonesho hayo kwa kuonesha mbinu mbalimbali alizozieleza kuwa zimesaidia wananchi kujifunza teknolojia bora katika mnyonyoro wa thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Akwilapo alitembelea Banda la Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Simiyu ambapo alipata fursa ya kukabidhi hati miliki za ardhi kwa baadhi ya wananchi wa Bariadi mkoani Simiyu waliokamilisha taratibu za kumilikishwa maeneo yao.
Akizungumza baada ya kukabidhi hati hizo, Dkt. Akwilapo aliwataka wananchi waliopokea hati hizo kuhakikisha wanazingatia masharti yote yanayoambatana na umiliki wa ardhi zao.
Maonesho na Sherehe za Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Mashariki, yamefungwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.