Habari

DKT. AKWILAPO ATEMBELEA WACHEZAJI WA ARDHI SPORTS WANAOSHIRIKI MASHINDANO YA SHIMIWI MOSHI

  • 22 Sep, 2026
DKT. AKWILAPO ATEMBELEA WACHEZAJI WA ARDHI SPORTS WANAOSHIRIKI MASHINDANO YA SHIMIWI MOSHI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amezungumza na wachezaji wa timu ya Ardhi Sports inayoshiriki mashindano ya SHIMIWI mkoani Kilimanjaro na kuwataka kuzingatia nidhamu wakati wote wawapo michezoni.

 

Dkt. Akwilapo amekutana na wachezaji hao Septemba 21, 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo.

 

Akizungumza na wachezaji hao, Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewaambia wachezaji wa Wizara yake kuwa, 

uwepo wao katika michezo hiyo bado ni watumishi wa uma hivyo wahakikishe wanazingatia maadili ya utumishi wa umma katika kipindi chote wawapo michezoni.

 

"Tuzingatia nidhamu katika michezo , michezo ni furaha, tudumishe michezo kama sehemu ya kazi na afya ya watumishi" amesema

 

Aidha, Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka wachezaji hao kujitahidi kwa hali na mali ili waweze kupata ushindi katika michuano hiyo na hatimaye kurejea na vikombe.

 

Wizara ya Ardhi katika michuano ya SHIMIWI mwaka huu inawakilishwa na wanamichezo 96 katika michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, riadha, karata, bao, kurusha tufe, darts na draft huku kauli mbiu ya SHIMIWI ikisema "Watumishi wa Umma Tuko Tayari Kwa AFCON 2027"