Habari

DKT. AKWILAPO ASHIRIKI MKUTANO WA TANO WA TUME YA PAMOJA YA KUDUMU KATI YA TANZANIA NA UGANDA

  • 16 Mar, 2026
DKT. AKWILAPO ASHIRIKI MKUTANO WA TANO WA TUME YA PAMOJA YA KUDUMU KATI YA TANZANIA NA UGANDA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo leo Machi 13, 2026 ameshiriki Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

 

Mkutano huo ulioanza Machi 3, 2026 kwa vikao vya wataalamu ulihitimishwa Machi 13, 2026 kwa Mawaziri wa nchi hizo mbili kukutana na kujadili uimarishaji ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.

 

Katika mkutano huo, Dkt Akwilapo alishiriki majadiliano yanayohusu sekta ya ardhi hususan eneo la uimarishaji wa mipaka ya kimataifa.

 

Aidha, wajumbe wa mkutano huo walipitia na kujadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa pamoja na kuweka mikakati ya kuendeleza ushirikiano katika sekta mbalimbali.

 

Mbali na sekta ya ardhi, mkutano huo pia umejadili masuala ya biashara na uchumi, uzalishaji wa nishati, mifugo na uvuvi, maji, usafirishaji pamoja na kilimo lengo likiwa  kukuza maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kuimarisha mahusiano ya kirafiki na kidiplomasia kati ya Tanzania na Uganda.

 

Mkutano huo ulisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayogusa wananchi wa pande zote mbili, hususan katika maeneo ya mipaka na sekta za uzalishaji.

 

Kamati ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Uganda imekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili, huku ikilenga kuimarisha diplomasia ya uchumi, biashara na maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Uganda.