Habari
DKT AKWILAPO ASHIRIKI KUMBUKIZI YA MIAKA 5 YA HAYATI JOHN POMBE MAGUFULI CHATO
- 18 Mar, 2026
Wilaya ya Chato mkoani Geita leo tarehe 17 Machi 2026 imekuwa kitovu cha kumbukizi ya miaka mitano tangu kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt John Pombe Joseph Magufuli.
Katika tukio hilo lililofanyika nyumbani kwa hayati Magufuli Chato, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt Leonard Akwilapo alishiriki pamoja na viongozi mbalimbali wa kitaifa kuadhimisha kumbukizi hiyo.
Mgeni rasmi katika kumbukizi hiyo alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt Emanuel Nchimbi. Kumbukizi hiyo pia zilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Masaju, pamoja na Naibu Spika Mhe. Daniel Sillo.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais Mstaafu Dkt Philip Mpango, Mawaziri Wakuu Wastaafu Kassim Majaliwa na Mizengo Pinda, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Stephen Wasira, pamoja na viongozi wengine wa chama na serikali.
Maadhimisho hayo yaliambatana na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge–Ngara, Mhashamu Severine Niwemugizi, ambapo waumini pamoja na viongozi walipata fursa ya kumuombea marehemu na kutafakari mchango wake kwa taifa.
Hayati Dkt John Pombe Joseph Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, na kumbukizi hizi za miaka mitano zimekuwa fursa kwa Watanzania kuendelea kumuenzi kwa mchango wake katika uongozi na maendeleo ya nchi.