Habari

DC UBUNGO AAGIZA WANANCHI KUPATIWA RASIMU YA MPANGO WA UENDELEZAJI UPYA SINZA

  • 11 Aug, 2026
DC UBUNGO AAGIZA WANANCHI KUPATIWA RASIMU YA MPANGO WA UENDELEZAJI UPYA SINZA

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ameagiza rasimu ya Mpango wa Uendelezaji Upya wa Eneo la Sinza jijini Dar es Salaam iandaliwe kwa lugha ya Kiswahili na kuwasilishwa kwa wananchi siku saba kabla ya majadiliano, ili wapate muda wa kuisoma, kuielewa na kuijadili kwa kina kabla ya kutoa maoni yao.

 

Msando ametoa agizo hilo Agosti 9, 2026, wakati akifungua kikao kazi cha kujadili mpango huo, akieleza kuwa mchakato huo unalenga kuanza upya ushirikishwaji wananchi kwa kuzingatia maagizo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Leonard Akwilapo pamoja na ule mpango kazi wa Serikali wa kuwahudumia wananchi.

 

Amesema, wananchi wameibua hoja zinazohitaji majibu ya kitaalamu na kisheria, ikiwemo namna umiliki wa ardhi na nyumba utakavyokuwa baada ya mpango kutekelezwa, utaratibu wa kushughulikia migogoro ya ubia pamoja na namna ya kuzuia watu kutumia fursa ya uendelezaji upya eneo la Sinza kwa manufaa binafsi.

 

"Elimu kwa wananchi na mpango ulio wazi ni msingi wa kufikia muafaka". Amesema

 

Akifafanua kuhusu mpango huo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. Deogratius Kalimenze, amesema uendelezaji upya wa Sinza ni sehemu ya kukabiliana na ongezeko la watu na mahitaji ya ardhi mijini wakati ardhi haiongezeki.

 

Kwa mujibu wa Bw. Kalimenze, miji inapaswa kuelekea katika ujenzi shadidi, ikiwemo majengo ya ghorofa, sambamba na kuboresha miundombinu na matumizi bora ya ardhi.

 

Amebainisha kuwa, Sheria ya Mipango Miji inaweka msingi wa ushiriki wa jamii katika upangaji matumizi ya ardhi, hivyo wananchi wanapaswa kushirikishwa katika mchakato huo ili kuweka mazingira bora ya ukuaji wa miji bila kuathiri maslahi ya jamii.

 

Kwa upande wao, wamiliki wa ardhi na nyumba wameunga mkono dhana ya uendelezaji upya, lakini wameomba kuwepo utaratibu wa wazi na ushirikishwaji wa kina. 

 

Bwana Evarist Maembe amesema, wamiliki washirikishwe kikamilifu ili kuondoa sintofahamu, huku Bi Christina Damas akitaka wataalamu kufanya tathmini na uthamini upya wa ardhi na mali zilizopo, pamoja na kuweka wazi aina ya majengo yatakayojengwa na utaratibu wa kulinda maslahi ya wamiliki, ikiwemo suala la fidia pale inapohitajika.

 

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mawela, Sinza, Dar es Salaam, Agosti 9, 2026, na kilihudhuriwa na viongozi, wataalamu na wamiliki wa ardhi na nyumba, ambapo washiriki walipata fursa ya kutoa maoni na kuuliza maswali kuhusu mpango huo, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa Serikali wa kupata maoni ya wananchi kabla ya hatua za utekelezaji.