Habari
DC KONDОA AWAPONGEZA WATAALAMU WA ARDHI, HATI 193 ZATOLEWA
- 04 Nov, 2026
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Bi. Fatma Almasi Nyangasa, amewapongeza wataalamu wa ardhi wa mkoa na wilaya kwa kazi kubwa na yenye ufanisi waliyoifanya katika zoezi la Kliniki ya Ardhi lililohitimishwa wilayani humo Oktoba 30, 2026.
Bi. Nyangasa ametoa pongezi hizo Novemba 03,2026 wakati akisomewa taarifa ya utekelezaji Kliniki ya Ardhi iliyofanyika kuanzia Oktoba 26 hadi 30, 2026 katika viwanja vya Halmashauri ya Mji wa Kondoa.
Bi. Nyangasa amesema ushirikiano wa wataalamu wa ardhi umewezesha wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za ardhi pamoja na kupatiwa hati miliki za maeneo yao.
“Tunawashukuru wataalamu wa ardhi kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha wananchi wetu kupata ufumbuzi wa migogoro na kupokea hati zao,” amesema.
Kliniki hiyo ya Ardhi imefanikisha kutolewa hati miliki 193 kwa wananchi, huku viwanja 3,647 vikisajiliwa katika mfumo wa kielektroniki wa e-Ardhi ndani ya Halmashauri ya Mji wa Kondoa.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewasihi wananchi waliopatiwa hati miliki za ardhi kupitia kliniki hiyo kuzitunza kwa uangalifu na kuzitumia kama nyaraka muhimu za kuthibitisha umiliki wa maeneo yao ili kuepuka migogoro ya ardhi.
“Ushahidi dhabiti ambao hauna kipengele ni kuwa na hati yako mkononi,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Bi. Happiness Mtutwa, amesema mbali na hati miliki 193 zilizotolewa, wataalamu wa ardhi wamepokea maombi 330 na kukamilisha michoro ya mipango miji 47 ambayo iko tayari kwa ajili ya wananchi kumilikishwa.
Bi. Mtutwa amesema, kuendelezwa kwa kliniki za ardhi ni mkakati muhimu wa kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi katika kupata huduma za ardhi kwa wakati.
“Sisi tuliona ni vizuri tuendeleze haya mazoezi ya kliniki za ardhi ili kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi wetu na kuhakikisha wanapata hati kwa urahisi na kwa haraka,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Bi. Zainab Harubu, amesema kliniki hiyo imesaidia wananchi kupata huduma za ardhi kwa haraka na kwa urahisi zaidi.
Ameeleza kuwa halmashauri hiyo ina mpango wa kutenga bajeti maalum kwa ajili ya kutatua changamoto za upimaji wa zamani wa mwaka 1985 pamoja na maeneo ya “dimension” katika mitaa ya Kitaruaini, Bicha, Mningani, Kilimamani na Maji ya Shamba.
Bi. Zainab amesema halmashauri itaingiza mpango huo katika bajeti yake ili kukamilisha upimaji na ramani zilizobaki, hatua itakayowezesha viwanja vyote husika kuingizwa katika mfumo wa e-Ardhi na kurahisisha utoaji wa huduma za umiliki wa ardhi kwa wananchi.