Habari

CHUO CHA ARDHI TABORA CHAHUISHA MITAALA KUENDANA NA DIRA 2050

  • 11 Jun, 2026
CHUO CHA ARDHI TABORA CHAHUISHA MITAALA KUENDANA NA DIRA 2050

Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) kimefanya mapitio kwa kushirikiana na wadau kuhuisha mitaala ya taaluma za Jiomatikia na Mazingira pamoja na mitaala mipya za Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS) na Mipangomiji na Vijiji ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira, maendeleo ya teknolojia na utekelezaji wa Dira 2050.

 

Akifungua kikao hicho Juni 10, 2026 mkoani Tabora, Mwenyekiti wa kikao na Mdhibiti Ubora Mwandamizi kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Bw. Ackles Bonaventure, amesema mapitio ya mitaala hiyo ni hatua muhimu ya kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanazalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani.

 

Bw. Bonaventure amesema NACTVET inaridhishwa na usimamizi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kusimamia na kuunga mkono juhudi za Chuo cha Ardhi Tabora kwa kuhakikisha wadau wanashirikishwa katika maboresho ya mitaala, pamoja na kazi kubwa inayoendelea ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia chuoni hapo.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora, Bw. Jeremiah Minja amesema maoni yaliyotolewa na wadau wameyapokea na watayafanyia kazi ili kukamilisha zoezi hilo na kuwasilisha NACTVET kwa wakati hatua inayosaidia kuandaliwa kwa mitaala inayozingatia matumizi ya teknolojia za kisasa na kuongeza ushindani wa wahitimu katika soko la ajira.

 

Akiwakilisha wadau walioshiriki mkutano huo, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Bi. Stella Sanga, amesema mitaala hiyo itasaidia kuzalisha wataalamu wenye maarifa, ujuzi na stadi zinazokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya maendeleo ya miji na vijiji.