Habari

ARDHI SPORTS YANG’ARA SHIMIWI, YATWAA VIKOMBE VINNE

  • 08 Oct, 2026
ARDHI SPORTS YANG’ARA SHIMIWI, YATWAA VIKOMBE VINNE

Timu ya Ardhi Sports imefanya vizuri katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali (SHIMIWI) 2026 kwa kutwaa vikombe vinne, ikiwemo ubingwa wa mpira wa miguu na mchezo wa Darts.

 

Mashindano hayo yaliyoshirikisha watumishi kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali nchini yamehitimishwa leo Oktoba 7, 2026 katika Viwanja vya Magereza, Moshi mkoani Kilimanjaro, huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikiibuka mshindi wa jumla.

 

Katika mashindano hayo, Ardhi Sports imefanikiwa kutwaa nafasi ya kwanza katika michezo ya mpira wa miguu na Darts, huku ikishika nafasi ya tatu katika michezo ya kurusha tufe na Draft, hivyo kufikisha jumla ya vikombe vinne.

 

Hafla ya kufunga mashindano na kukabidhi vikombe imefanywa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ambaye alikuwa mgeni rasmi.

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amewapongeza wachezaji wa Ardhi Sports kwa kujituma, kuonyesha nidhamu na ushindani uliowawezesha kufanya vizuri na kutwaa vikombe katika michezo mbalimbali.

 

Dkt. Akwilapo amesema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za wachezaji pamoja na ushirikiano uliopo miongoni mwa watumishi wa Wizara, akiwataka wanamichezo hao kuendelea kudumisha kiwango hicho katika mashindano yajayo.

 

Aidha, amewataka wanamichezo wa Ardhi Sports kutumia michezo kama sehemu ya kuitangaza vyema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, huku wakiendelea kudumisha moyo wa ushindani, mshikamano, nidhamu na uzalendo.

 

Kaulimbiu ya Mashindano ya SHIMIWI 2026 ilikuwa “Watumishi wa Umma Tupo Tayari kwa AFCON 2027”, ikiwa na lengo la kuhamasisha maandalizi, mshikamano na ari kuelekea michuano hiyo mikubwa ya soka barani Afrika.

 

Mashindano ya SHIMIWI huwakutanisha watumishi wa Serikali kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha afya, mshikamano, nidhamu na mahusiano mema ya kikazi miongoni mwa watumishi.