Habari
ARDHI SPORTS CLUB YANG’ARA, YAILAZA MIFUGO 1–0
- 07 Sep, 2026
Timu ya Ardhi Sports Club imeanza kuonyesha makali kuelekea Mashindano ya SHIMIWI 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Mifugo Sports Club katika mchezo wa kirafiki uliochezwa leo katika Uwanja wa Kilimani mkoani Dodoma.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Ardhi Sports Club ilionyesha kiwango kizuri na nidhamu ya mchezo, huku Philipo Mavika akiwa shujaa wa timu hiyo baada ya kufunga bao pekee lililoipa Ardhi ushindi.
Ushindi huo umeongeza morali kwa wachezaji na benchi la ufundi, huku maandalizi yakiendelea kwa kasi kuelekea Mashindano ya SHIMIWI yanayotarajiwa kuanza Septemba 20, 2026, mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza baada ya mchezo, Mavika amesema ushindi huo ni chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii, akisisitiza kuwa timu bado inaendelea kujipanga ili kufanya vizuri katika mashindano hayo.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Timu Bw.Abdalla Mussa Ngware amesema michezo ya kirafiki ni muhimu katika kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuwaweka wachezaji katika utayari wa ushindani.
Amewataka wachezaji waliopo mikoani kushiriki mazoezi kwa nguvu zao zote ili Wizara ikafanye vizuri katika mashindano ya shimiwi.
Ardhi Sports Club sasa inaendelea na maandalizi huku ikibeba matumaini ya kufanya vizuri na kuiwakilisha vyema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika SHIMIWI 2026.