Habari
AKWILAPO ASISITIZA USHIRIKIANO WA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI KUKUZA SEKTA YA MILKI
- 20 Nov, 2026
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. DKt Leonard Akwilapo, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kukuza sekta ya Milki nchini, akieleza kuwa sekta hiyo ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, uzalishaji wa ajira, ujenzi wa utajiri na maendeleo ya viwanda.
Mhe Dkt. Akwilapo amesema hayo leo Novemba 20, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi wa maonesho ya TAREX 2026, yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba katika ukumbi wa Super Dome Dar es Salaam.
Amesema, sekta ya Milki ina nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga Tanzania yenye uchumi imara, jumuishi na shindani ambapo ameweka wazi kuwa, kufikia azma hiyo kunahitaji uwekezaji katika miji iliyopangwa vizuri, makazi endelevu, nyumba zinazomudu gharama zake pamoja na mifumo madhubuti ya usimamizi wa ardhi.
"Sekta ya Milki haiishii katika ununuzi na uuzaji wa ardhi na majengo pekee, bali inaunganisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo ujenzi, huduma za kifedha, bima na miundombinu, huku ikichangia upatikanaji wa makazi bora na ya kutosha kwa wananchi". Amesema
Aidha, Mhe Dkt. Akwilapo amebainisha kuwa Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuhamasisha mitaji, teknolojia, ubunifu na utaalamu ili kuongeza kasi ya maendeleo ya sekta ya Milki hivyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia sera zinazofaa, kuboresha mifumo ya usimamizi wa ardhi, kuimarisha utoaji huduma na kuhakikisha usalama wa milki.
Akifafanua zaidi, amesema hatua hizo zinalenga kuongeza uwazi na uhakika katika miamala ya ardhi, kujenga imani ya wawekezaji na kuhakikisha ardhi inatumika kama rasilimali yenye tija kwa maendeleo ya taifa.
Amewahimiza wadau hao wa sekta ya milki kushirikiana na Serikali katika kujenga nyumba za gharama nafuu, kuandaa maeneo yenye huduma muhimu na kubuni mifumo ya mikopo ya nyumba inayowawezesha Watanzania wengi kumudu umiliki wa makazi.
Vile vile, amewataka wananchi na wawekezaji kwa ujumla kufanya uhakiki wa kina kabla ya kuingia katika miamala ya ardhi na Milki ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.