Habari

AKWILAPO ASHIRIKI KIKAO CHA 14 CHA MAWAZIRI WA ARDHI RCMRD NAMIBIA

  • 18 Nov, 2026
AKWILAPO ASHIRIKI KIKAO CHA 14 CHA MAWAZIRI WA ARDHI RCMRD NAMIBIA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dk Leonard Akwilapo ameshiriki kikao cha 14 cha Kituo cha Kikanda cha Rasilimali za Ramani kwa Maendeleo (Regional Center for Mapping of Resources for Development - RCMRD) kilichofanyika Mjini Swakopmund, Mkoa wa Irongo nchini Namibia kuanzia Novemba 16 hadi 17, 2026.

 

Kikao hicho cha siku mbili kimetanguliwa na vikao viwili vya Wataalam ambavyo ni Kamati ya Wataalam inayojumuisha Wakurugenzi wa Upimaji kutoka nchi wanachama pamoja na kile cha Baraza la Uongozi linalojumuisha Makatibu Wakuu kutoka Wizara zinazosimamia masuala ya ardhi kutoka katika nchi wanachama.

 

Aidha, kikao hicho kimefanya kazi ya kupitia na kuidhinisha Taarifa ya utekelezaji wa kazi za kituo cha RCMRD kwa mwaka 2026, Mpango Mkakati wa kituo cha RCMRD 2027-2030, Mpangokazi pamoja na Bajeti ya kituo kwa mwaka 2027.

 

Katika kikao hicho jumla ya nchi kumi na tano (15) zimeshiriki kati ya nchi ishirini (20) wanachama na nchi tano hazijashiriki ambazo ni Ethiopia, Shelisheli, Somalia, Sudani Kusini na Sudani.

 

Vile vile, Kituo cha RCMRD kimetoa taarifa ya washindi katika shindano la uaandaaji ramani miongoni mwa nchi wanachama ambapo Mshindi wa jumla amepatikana kutoka Dar es Salaam, Tanzania anayejulikana kwa jina la Monata Sharisho aliyepata zawadi ya Euro 4000.

 

Washindi wengine wametoka katika nchi zifuatazo za Kenya Euro 3000, Zimbabwe Euro 3000, Madagascar Euro 2000, Rwanda Euro 2000 pamoja na Malawi Euro 2000.