Habari
AKWILAPO APONGEZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KISANGIRO
- 23 Sep, 2026
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amekagua utekelezaji wa Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo lililokuwa Shamba Na. 2 Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, na kupongeza hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Dkt. Akwilapo alifanya ukaguzi huo Septemba 21, 2026, katika eneo la mradi lililopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, ambapo aliwapongeza waratibu wa mradi kwa juhudi wanazofanya kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa.
Alisema Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inalenga kuhakikisha maeneo mbalimbali nchini yanapangwa na kupimwa ili wananchi waweze kuishi katika maeneo yaliyopangwa na yenye miundombinu na huduma muhimu.
“Sisi kama Wizara tuna lengo kwa nchi nzima kuhakikisha tunapanga ili wananchi waishi maeneo yaliyopangwa. Hilo ndilo lengo na maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhakikisha ardhi yote nchini inapangwa na kupimwa,” alisema Dkt. Akwilapo.
Aidha, alieleza kuwa, pamoja na Wizara kushughulikia masuala ya migogoro ya ardhi, ina wajibu mpana zaidi wa kuhakikisha maendeleo ya makazi yanapangwa vizuri ili kurahisisha upatikanaji huduma muhimu kama maji na umeme, pamoja na miundombinu ya barabara.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Rehema Mdee, alisema katika utekelezaji wa mradi huo ofisi yake ilipokea Shilingi milioni 300 kutoka Wizara ya Ardhi kwa ajili ya awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mradi wa Kupanga, Kupima, Kufungua Barabara, Kumilikisha na Kutwaa Ardhi.
Alisema fedha hizo zilitumika katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi unaohusisha eneo lenye ukubwa wa ekari 227 lililopo mbele ya eneo la mradi.
Alisema, utekelezaji wa mpango huo unalenga kuwezesha eneo hilo kuwa mji unaojitegemea, ambao kwa mujibu wa mpango wake umepewa jina la Kisangiro Satellite City.