Habari

AKILI UNDE KUCHOCHEA MAPINDUZI YA UPIMAJI WA ARDHI KISASA

  • 23 Nov, 2026
AKILI UNDE KUCHOCHEA MAPINDUZI YA UPIMAJI WA ARDHI KISASA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amesema matumizi ya Sayansi ya Kijiografia na Akili Unde (Artificial Intelligence) katika kutafuta, kukusanya na kuchambua takwimu za kijiografia yatasaidia kuboresha shughuli za upimaji wa ardhi nchini, kuongeza ufanisi na kuchochea ubunifu unaoendana na maendeleo ya teknolojia duniani.

 

Mhe. Mmuya amesema hayo jijini Mwanza, wakati akifungua Kongamano la Wapima Ardhi Tanzania pamoja na Mkutano Mkuu wa 30 wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Ardhi Tanzania (IST), akieleza kuwa matumizi ya teknolojia hizo ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya upimaji na usimamizi wa ardhi ili kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo.

 

Amesema kauli mbiu ya kongamano hilo inaakisi utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayohitaji matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya sekta mbalimbali nchini.

 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Wapima Ardhi kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwa kutumia maarifa na mifumo ya kisasa katika kutafuta na kuchakata taarifa za kijiografia zitakazosaidia kufanya maamuzi sahihi katika shughuli za upimaji na usimamizi wa ardhi.

 

Kongamano la mwaka huu limeongozwa na kauli mbiu isemayo: “Sayansi ya Kijiografia, Akili Unde na Upimaji Ardhi wa Kisasa: Kuchochea Ubunifu kwa ajili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.”