Habari

AGIZO LA WAZIRI SILAA LA KUHAMISHIA HUDUMA ZA ARDHI OFISINI KWAKE LAANZA KUTEKELEZWA DODOMA

  • 03 Jun, 2024
AGIZO LA WAZIRI SILAA LA KUHAMISHIA HUDUMA ZA ARDHI OFISINI KWAKE LAANZA KUTEKELEZWA DODOMA

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kutekeleza agizo la Waziri Mhe. Jerry Silaa alilolitoa Mei 28, 2024 baada ya kufunga masijala ya Ardhi jijini Dodoma.

 

Zoezi la Ardhi Kliniki limeanza Juni 3, 2024 katika Ofisi za Halmashauri ya jiji la Dodoma ambapo Waziri Silaa alitoa maelekezo msijala hiyo irudishwe Ofisini kwake iwe chini ya usimamizi na uangalizi wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga ili kuwahudumia wananchi kutatua changamoto za ardhi zinazowakabili.

 

“Watendaji wote wakae sehemu moja, mwananchi kama anashida ahudumiwe katika eneo moja. Mhe. Jerry Willam Silaa amelionge hili Bungeni, ameliongea mara kwan mara katika mikutano yake lengo la msingi ni kuwahudumia wananchi katika eneo moja na wasipate adha ya nenda ofisi fulani, wala njoo kesho hii ndiyo dhana halisi ya kituo kinmoja jumuishi (one stop centre). Hapa ni watu wa ardhi bila kuangalia mipaka ya utawala,” amesema Mhandisi Sanga. 

 

Zoezi hilo la Kliniki litafanyika kwa muda wa wiki mbili ambapo wananchi watahudumia kwa kutatua migogoro yao na kupatiwa hati miliki ya ardhi yao kwa kuzingatia wananchi wana migogoro mingi ambayo inatokana ama kwa kutapeliwa au ardhi yao kupewa zaidi ya mtu mmoja na baadhi ya watumishi wasio waadilifu.

 

Mamia ya wananchi wamemiminika katika viwanja vya Ofisi za Halmashauri ya jiji la Dodoma kutatua madhila ya ardhi yanayowakabili ili watumie ardhi na muda wao kwa shughuli za kiuchumi kujiletea maendeleo.

 

Akizungumzia zoezi hilo linaloendelea jijini Dodoma, Katherine Mwimbe Mwekezaji na Mkurugenzi wa Taasisi ya Domaiya Estate Dodoma Tanzania inayojishughulisha na usindikaji wa mvinyo na huduma za hoteli ni miongoni mwa waliopata huduma kwenye Kliniki ya Ardhi inayoendelea jijini Dodoma ambapo amesema ameridhishwa na huduma zinazotolewa katika zoezi hilo.

 

“Tumekuwa na changamoto za ardhi katika uwekezaji wetu, tumepata simu tukakaribishwa katika kambi hii maalum inayozungumzia masuala ya ardhi, tuliambiwa tufike saa 2:30, tumefika kwa wakati mara moja tumepata huduma tunayohitaji, tumekuja na nyaraka zetu. Vitu vimefanyiwa kazi, tunapata matumaini na tuanweza kuendelea na uwekezaji na biashara” amesema Mwimbe.

 

Mwimbe ameongeza “Sisi kama kampuni ya kimataifa tumepata huduma nzuri, hiyo imetupan sana moyo, naamini tunaweza kwenda kufanya maendeleo zaidi hasa katika sekta ya mvinyo hapa Dodoma.

 

Zoezi hilo linaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga, Naibu Katibu Mkuu Lucy Kabyemera, Kamishna wa Ardhi Methew Nhonge, watendaji wa wizara hiyo pamoja na watendaji wa Ardhi mkoa wa Dodoma.