Habari

AGIZO LA RAIS KLINIKI YA ARDHI KILINDI LIMEANZA KUTEKELEZWA

  • 07 Mar, 2025
AGIZO LA RAIS KLINIKI YA ARDHI KILINDI LIMEANZA KUTEKELEZWA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemera amewataka wananchi wa wilaya ya Kilindi kuheshimu mpango wa matumizi Bora ya ardhi ili kuepuka kuwa na migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo. 

 

Naibu Katibu Mkuu Kabyemera ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Mswaki wilayani Kilindi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan akiwa ziarani mkoani Tanga katika wilaya ya Kilindi.

 

Mhe. Rais katika hotuba yake alimuagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi kuhakikisha huduma ya Kliniki ya Ardhi inafika katika wilaya hiyo ili kukomesha migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikisababisha mivutano kwa wananchi wa Kilindi hususani wakulima na wafugaji.