Habari

WAZIRI AKWILAPO AITAKA MIKOA NA WILAYA KUTENGA MAENEO YA VIWANDA

  • 08 Aug, 2026
WAZIRI AKWILAPO AITAKA MIKOA NA WILAYA KUTENGA MAENEO YA VIWANDA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo ameitaka mikoa na wilaya nchini kuhakikisha zinatenga na kuandaa maeneo maalumu yatakayotumika kwa ajili ya kuanzisha kongani za viwanda.

 

Amesema upangaji mzuri wa matumizi ya ardhi ni muhimu katika kuvutia wawekezaji kwa kuwa mwekezaji anahitaji eneo lililotengwa na kutambuliwa kwa matumizi husika kabla ya kuanzisha shughuli zake.

 

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati alikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa shule ya awali na msingi katika Kitongoji cha Mwankola, Kata ya Lagangabilili pamoja na kusikiliza kero za wananchi katika Kijiji cha Simiyu kata ya Migato wilayani itilima mkoa wa Simiyu tarehe 7 Agosti 2026 Dkt. Akwilapo amesema hatua hiyo pia inalenga kuzuia migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya makazi, shughuli za kilimo, viwanda na matumizi mengine yanayohitaji maeneo maalumu.

 

Aidha, Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameeleza kuwa, Wizara yake imejipanga kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maeneo yao yanasimamiwa kwa kuzingatia sheria.

 

Amewataka wananchi wa Itilima kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazohusu umiliki na matumizi ya ardhi ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na migogoro ya ardhi.

 

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha ameeleza kuwa, mkoa wa Simiyu hususan wilaya ya Itilima wanatambua umuhimu wa ardhi hasa katika kumilikisha wananchi, taasisi na vijiji lengo likiwa kuepuka migogoro ya ardhi.

 

Mkuu wa wilaya ya Itilima Bi. Anna Gidarya amesema halmashauri ya wilaya ya Itilima ina lengo la kuandaa hati milki za viwanja vyote 1,604 vilivyopangwa ambapo hadi kufikia juni 2026 jumla ya hati milki 506 zimeandaliwa na kusajiliwa.

 

''Hati za viwanja vilivyosalia havijamilkishwa kwa vile wamiliki hawajalipia gharama za uandaaji wa milki hizo''. Amesema Bi. Gidarya.

 

Ziara ya Dkt Akwilapo wilayani Simiyu ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwapeleka mawaziri katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyoahidiwa kwa wananchi wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akiomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.