Habari

WATANZANIA WATAKIWA KUOMBA HATIMILIKI

  • 06 Aug, 2026
WATANZANIA WATAKIWA KUOMBA HATIMILIKI

Serikali imewataka Watanzania wote waliotimiza vigezo vya kisheria vya kumiliki ardhi kuanza mchakato wa kuomba Hatimiliki ili kulinda haki zao za umiliki na kuongeza thamani ya ardhi wanayoimiliki.

 

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, alipotembelea banda la Wizara ya Ardhi katika Maonesho ya 32 ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.

 

Mhe. Mmuya amesema hafurahishwi kuona Mtanzania anayestahili kumiliki ardhi akikosa Hatimiliki wakati taarifa zake za umiliki zinathibitishwa kwa mujibu wa sheria. Hivyo, amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanashughulikia kwa haraka maombi yote yaliyokamilika ili wananchi wapate hati kwa wakati.

 

Aidha, amewasisitiza watumishi hao kuongeza umakini katika uhakiki wa taarifa za waombaji kabla ya kutoa hati, ili kuhakikisha hati zinatolewa kwa wahusika halali na kuepusha migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza kutokana na makosa katika mchakato wa umilikishaji.

 

Amesema utoaji wa Hatimiliki ni moja ya hatua muhimu za kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi, kuchochea maendeleo ya wananchi na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia matumizi rasmi ya ardhi.