Habari
WANANCHI WAHAMASISHWA KUTEMBELEA BANDA LA WIZARA YA ARDHI KATIKA MAONESHO YA NANENANE NZUGUNI DODOMA
- 06 Aug, 2026
Wananchi wamehimizwa kutembelea Banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ili kupata huduma mbalimbali za ardhi pamoja na elimu kuhusu umiliki salama wa ardhi na maendeleo ya makazi.
Akizungumza katika maonesho hayo, Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Bi. Happiness Mtutwa, amesema Wizara imejipanga kikamilifu kuwahudumia wananchi kwa kutoa huduma na elimu kuhusu upangaji na upimaji wa ardhi, umilikishaji wa ardhi, utoaji wa hati za miliki, pamoja na ushauri wa kitaalamu unaolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi nchini.
Bi. Mtutwa amewahimiza wananchi kutumia vyema fursa hiyo kwa kutembelea banda la Wizara ili kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya ardhi, kutatua changamoto zinazowakabili na kujionea maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali katika utoaji wa huduma za sekta ya ardhi.
Ameongeza kuwa maonesho ya Nanenane kwa Kanda ya Kati yanashirikisha mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro, ambapo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi, zikiwemo Chuo cha Ardhi Tabora, Chuo cha Ardhi Morogoro na Chuo cha Ardhi TGNC Dodoma, zinatoa elimu kuhusu fursa za masomo, kozi na taaluma mbalimbali zinazotolewa katika sekta ya ardhi.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kuwakaribisha wananchi wote kutembelea banda lake ili kupata huduma mbalimbali kwa wakati, ushauri wa kitaalamu na elimu itakayowasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu umiliki na matumizi ya ardhi.
Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nanenane mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: "Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."