Habari

SANGA: MAADILI, WELEDI NA UWAJIBIKAJI VIWE MSINGI WA UTUMISHI WENU

  • 07 Aug, 2026
SANGA: MAADILI, WELEDI NA UWAJIBIKAJI VIWE MSINGI WA UTUMISHI WENU

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amewataka waajiriwa wapya wa Wizara hiyo kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, huku wakizingatia maadili ya utumishi wa umma ili kulinda heshima na taswira ya Wizara.

 

Mhandisi Sanga ametoa kauli hiyo tarehe 6 Agosti, 2026 wakati akifungua mafunzo ya utambulisho wa kazi (Induction Programme) yaliyofanyika katika Ukumbi wa St. Gaspar, jijini Dodoma.

 

'Serikali imewaamini na kuwapa dhamana ya kulitumikia taifa. Kila mmoja ahakikishe anaitendea haki nafasi aliyopewa kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na uwajibikaji," amesema Mhandisi Sanga.

 

Amesema, anatarajia ujio wa waajiriwa hao utaleta matokeo chanya kwa Wizara na Taifa kwa ujumla, huku akiwataka kuwa chachu ya ubunifu, utendaji na mijadala yenye kujenga kuhusu kazi badala ya kujadili watu.

 

Amemshukuru Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiamini Wizara kwa kuidhinisha ajira za watumishi wapya 137 mwaka huu, baada ya zaidi ya watumishi 400 kuajiriwa mwaka uliopita.

 

Kwa mujibu wa mhandisi Sanga, hatua hiyo inaonesha imani kubwa ya Serikali kwa Wizara na kwa waajiriwa hao, hivyo amewataka kuitendea haki fursa waliyopewa kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu.

 

Awali, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Salome Kessy, alimueleza Katibu Mkuu kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea waajiriwa wapya uelewa wa majukumu yao, maadili ya utumishi wa umma pamoja na utendaji wa Wizara, ili waanze kazi wakiwa na weledi na ufanisi.

 

Jumla ya waajiriwa wapya 137 wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutoka kada mbalimbali wanashiriki mafunzo ya utambulisho wa kazi (Induction Programme) yenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu majukumu yao, maadili ya utumishi wa umma, sheria, kanuni na taratibu za Serikali sambamba na mfumo wa utendaji wa Wizara ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.