Habari

MMUYA AINGILIA KATI MGOGORO WA ARDHI MONDULI, SERIKALI KUKAA NA MWEKEZAJI

  • 08 Aug, 2026
MMUYA AINGILIA KATI MGOGORO WA ARDHI MONDULI, SERIKALI KUKAA NA MWEKEZAJI

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, ameanza mchakato wa kutafuta suluhisho la mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 15 kati ya wananchi wa Kijiji cha Oldonyo, Wilaya ya Monduli, wananchi wa Kijiji cha Lobusoit A, Wilaya ya Simanjiro na mwekezaji wa Shamba Na. 24 la Maasai Steppe Conservancy Ltd.

 

Akizungumza na mamia ya wananchi katika Kijiji cha Oldonyo leo Agosti 7, 2026, Mhe. Mmuya alisema hatua ya kwanza ya Serikali ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu historia ya umiliki wa eneo hilo ili kupata msingi wa kudumu wa kutatua mgogoro huo.

 

Alisema mwekezaji anamiliki kihalali hekta 3,425, lakini bado kuna madai ya ziada ya hekta 870.3 kutoka upande wa Monduli na hekta 1,778.3 zinazodaiwa na wananchi wa Simanjiro, jambo linalohitaji uchambuzi wa kina wa kisheria na kiutawala.

 

Naibu Waziri Mmuya alisisitiza kuwa Serikali haitafanya uamuzi bila kusikiliza pande zote hadi hapo ukweli uwekwe bayana na suluhisho kupatikana kwa kuzingatia sheria, haki na maslahi ya wananchi.

 

Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mhe. Isack Copriano, alisema wananchi wa Monduli na Simanjiro wanahitaji kurejeshewa maeneo wanayoamini ni haki yao, huku akieleza imani yake kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itafikia uamuzi utakaorejesha amani na kuondoa sintofahamu iliyodumu kwa miaka mingi.

 

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyo, Saitoti Mwatuni, alisema mgogoro huo umeathiri shughuli za wafugaji kwa muda mrefu na kuiomba Serikali kuharakisha hatua za kuupatia ufumbuzi ili wananchi waendelee kutumia ardhi yao kwa amani.

 

Hatua hiyo ni sehemu ya msimamo wa Serikali wa kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa njia ya mazungumzo, kuzingatia sheria na ushirikishwaji wa wananchi, ili kurejesha utulivu na matumizi bora ya ardhi katika maeneo yenye migogoro nchini.