WARASHIMISHAJI WAONYWA KUFANYA KAZI BILA KUZINGATIA WELEDI
Posted On: 09th September, 2020
Warasimishaji
wanaofanya kazi za upangaji na upimaji makazi holela katika mitaa mbalimbali ya
mkoa wa Arusha wameagizwa kufanya kazi hizo kwa kuzingatia weledi na maadili ya
taaluma zao ili kazi zao zikidhi vigezo vya upangaji na upimaji vilivyowekwa
kwa mujibu wa sheria.
Maagizo
hayo yametolewa na Bwn PrayGod Shao, Kiongozi wa kikosi kazi maalum cha Wizara
ya Ardhi, kilichoundwa kwa ajili ya kukwamua changamoto za urasimishaji mkoani
Arusha wakati alipokuwa akikagua kazi za upimaji katika Mtaa wa Engosowashi
Kata ya Moshono na Mtaa wa Olmokea Kata ya Sinoni.
Akiwa
katika ukaguzi wa uwekaji vigingi (beacons) na uandaaji wa ramani za upimaji
(survey plan), Bwn Shao amesema amegundua warasimishaji wengi hawafuati sheria
na kanuni za upimaji kwani badala ya kupanda vigingi kwenye mipaka ya viwanja
wamevikusanya na kuvifungia ndani ya nyumba kitu ambacho ni kinyume na sheria
ya upimaji.
‘Vigingi
(beacons) vinatakiwa vichimbiwe chini ardhini ili vitumike kama alama ya kubainisha
mpaka wa kiwanja kimoja na kingine na siyo kuhifadhiwa ndani, alisema Shao.’
Aidha,
Bwn Shao aliongeza kwamba, mbali na kuvifungia ndani vigingi walivyopaswa
kuvichimbia ardhini, bado wameweka alama hewa za upimaji kwenye ramani (Survey
plan) ambapo utakuta ramani inaonesha kiwanja kimewekewa vigingi ila ukifika
kwenye kiwanja husika hakuna uhalisia wa vigingi hivyo.
Alisisitiza
kwamba, serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya kusimamia ardhi haiwezi kufumbia
macho udanganyifu kama huo unaofanywa na warasimishaji wa kuweka alama hewa za
upimaji katika viwanja kwa sababu mwisho utasababisha migogoro isiyo ya lazima.
Ni lazima sheria na miongozo ya upimaji izingatiwe kwa kuhakikisha kila kiwanja
kiwekewe vigingi vyake na ramani inasomeka vivyo hivyo.
Kwa
upande wake msimamizi wa Kampuni ya Savei Consult moja kati ya Kampuni
zinazofanya urasimishaji katika mkoa wa Arusha Bwn Bryson Michael alisema,
uwekaji vigingi (beacons) kwenye mitaa yote ya urasimishaji unasua sua kutokana
na mwitikio mdogo wa wananchi wa kulipa gharama za upimaji kiasi cha Tsh.
150,000 kilichowekwa na Serikali.
Bryson
alisema, kazi ya utambuzi wa makazi katika mitaa mitatu kwenye Kata ya Moshono
aliyopewa kurasimisha imeshafanyika ambapo michoro ya mipangomiji kwa mitaa
hiyo imeshaandaliwa na hivyo upimaji unaendelea.
Kwa
kuona umuhimu wa kazi ya urasimishaji mkoani Arusha, Wizara ya Ardhi iliunda
kikosi kazi maalum cha kufuatilia na kukwamua changamoto za urasimishaji, na
kilianza kazi tangu Agosti 17, mwaka 2020 ambapo kufikia Agosti 30, mwaka huu
2020 makampuni yote yaliyokuwa yanafanya urasimishaji katika Mkoa wa Arusha
yanapaswa kukamilisha kazi zao zote.