Makampuni ya watu binafsi yanayofanya kazi za urasimishaji katika mitaa mbalimbali ya jiji la Arusha yameagizwa kukamilisha kazi zao zote ifikapo Agosti 30 mwaka huu 2020, vinginevyo Serikali haitawafumbia tena macho hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bibi Mary G. Makondo alipokutana na makampuni hayo jijini humo na kuwaeleza mikakati ya Wizara katika kukwamua kero za urasimishaji, zoezi ambalo linatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti, 2020.
‘Serikali
inapotoa miongozo ni lazima isimamiwe na itekelezwe ipasavyo. Unaposhindwa
kusimamia mkataba wako katika kutoa huduma unakosa uaminifu. Kufanya kazi kwa
kusimamia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ni kuwekeza kwa yule aliyekupa
hiyo kazi na kwa Serikali iliyokuamini na kukupa fursa, alisema Bibi Mary.’
Aliongeza
kwamba, lengo la Wizara kuanzisha urasimishaji lilikuwa ni kupandisha hadhi na
kuondoa makazi holela kwenye maeneo yaliyokwisha endelezwa tayari lakini, kazi
hii ilipaswa kuwa na ukomo na siyo kazi endelevu. Zoezi hili lilipaswa
lifanyike kwa malengo maalum na matunda yake yaonekane.
Katika
jiji la Arusha pekee, kuna jumla ya makampuni 25 yanayofanya kazi za upangaji
na upimaji katika mitaa 120. Kati ya mitaa hiyo yote, hakuna mtaa hata mmoja
ambao kazi za urasimishaji zimekamilika licha ya kwamba wananchi wamechangia
hela zao kwa ajili ya kurasimishiwa maeneo yao. Hali hiyo ndiyo inayopelekea
Serikali kupitia wizara ya Ardhi kuchukua hatua za ziada kuona ni kwa namna
gani kero hizo zinaweza kukwamuliwa.
Awali,
akizungumza na makampuni hayo yanayorasimisha makazi holela katika jiji la
Arusha Kamishna Msaidizi mkoa wa Arusha Bwn Leo Komba alisema; utendaji kazi wa
makampuni hayo hauridhishi, wamesababisha malalamiko mengi sana kutokana na
kazi zao kutokukamilika kwa wakati. Aliongeza kwamba, makampuni mengi yanapita
mitaani kuhamasisha wananchi kulipia gharama za urasimishaji na fedha hizo
wanachukua lakini kasi ya kuwapimia ili wamilikishwe ni ndogo sana.
‘Serikali
inachohitaji ni kuona wananchi wanapatiwa hati, wanarasimishiwa makazi yao na
kua na hakika ya usalama wa milki zao. Matarajio ya Serikali ni makubwa sana
hadi kuingia mkataba na nyie warasimishaji, alisema Kamishna komba’.
Aidha,
Komba aliweka wazi kwamba, ofisi yake imepokea maagizo kutoka kwa Katibu Mkuu
wizara ya Ardhi kwamba hadi kufikia tarehe 30, Agosti mwaka huu 2020, kila
kampuni ambayo inafanya kazi ya urasimishaji katika jiji la Arusha iwe
imekamilisha kazi zake zote. Alitoa rai kwa makampuni yote ambayo tayari
yalishaingia mkataba na wananchi kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha
kazi hizo vinginevyo watakuwa na wakati mgumu kwani hata yeye amechoka kupokea
malalamiko ya urasimishaji.
Katika kuhakikisha kwamba kero zote za urasimishaji zinakwamuliwa, Wizara ya Ardhi imeunda kikosi kazi maalum kitakachosaidia kukwamua kero hizo ili makampuni hayo yasikwame kukamilisha kazi zao kwa muda waliopewa. Kikosi kazi hicho kinachoongozwa na Bwn. Praygod Shao amabaye ni Afisa Ardhi, kitakuwa kinapitia kazi zote zinazozalishwa na makampuni hayo ya urasimishaji na kutoa msaada wa kitaalam pale panapohitajika ili kuwaongezea kasi ya upimaji ambayo ndiyo lengo kuu la urasimishaji. Kama upimaji ukikamilika vizuri, umilikishaji hautakuwa ni tatizo kwa sababu kila mwananchi anatamani apimiwe ili amilikishwe kwa mujibu wa sheria.
© 2021 All Rights Reserved.
Site Map
Staff Mail
Designed and Developed bylbl_ega_nam (e-GA) and Contents Managed by Ministry of Lands, Housing and Human Settlements Development