WATENDAJI SEKTA YA ARDHI WAASWA KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO
Posted On: 04th October, 2020
Na:
Eliafile Solla
Watendaji
wa sekta ya Ardhi katika Halmashauri ya Manyoni mkoani Singida, wametakiwa
kufanya kazi kwa ushirikiano na umoja ili kutekeleza majukumu
yao kwa urahisi zaidi. Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu kamishna wa Ardhi msaidizi
mkoa wa Singida Bwn Speratus Ruteganya, katika kampeni maalum iliyozinduliwa na
Wizara ya siku ya elimu ya mlipa kodi ambayo hutekelezwa kila siku ya Ijumaa.
Akizungumza
na kikosi kazi maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kilichofika Wilayani Manyoni kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu kodi ya
pango la Ardhi, Ruteganya alisema umoja na ushirikiano ndiyo nguzo pekee ya
kufikia malengo katika sekta ya Ardhi. Aliongeza kwamba, wananchi wanachohitaji
ni elimu tuu kwani wakielimika kodi itapatikana pamoja na taarifa muhimu za
umiliki.
Kwa
upande wake kiongozi wa kikosi kazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Bwn Adam Komba alisema, lengo la Wizara kuanzisha siku ya elimu kwa
mlipa kodi ni kuhakikisha wananchi wanapewa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi
pamoja na kuboresha taarifa zao za umiliki. Alisisitiza kwamba, kutokana na
mabadiliko ya teknolojia hasa kwenye utoaji wa huduma, Wizara ina mpango wa
kuboresha mifumo yake ya utoaji huduma hivyo pamoja na kutoa elimu kuhusu kodi
ya pango la Ardhi pia zoezi linalenga upatikanaji wa taarifa muhimu za kila
mmiliki wa kipande cha Ardhi.
Naye
afisa Ardhi mteule wa Wilaya ya Manyoni Bi. Zamzam Seif, aliishukuru Wizara ya
Ardhi kwa hatua mathubuti iliyochukua ya kuboresha taarifa za wamiliki Ardhi na
pia kampeni ya siku ya elimu ya mlipa kodi. Zamzam alisema, kitendo cha Wizara
kutuma kikosi kazi Wilayani hapo na kimewapa moyo sana na nguvu mpya ya kufanya
kazi.
Siku ya elimu ya Mlipa kodi
ni kampeni maalum iliyoanzishwa na Wizara ya Ardhi ambapo, kila siku ya Ijumaa
kikosi kazi kitakuwa kinapita mitaani kutoa elimu nyumba kwa nyumba ili
kuhakikisha wamiliki wa Ardhi wanajua sheria, kanuni, taratibu na miongozo
inayoisimamia sekta ya Ardhi. Pamoja na hayo, pia lengo ni kuhakikisha Wizara
inajenga ukaribu zaidi na wamiliki wa Ardhi na kuona namna bora ya kutatua
changamoto mbalimbali za sekta ya Ardhi kwa ujumla.