Huduma Zetu

Uthamini

Uthamini

1. Uthamini ni nini?

Uthamini ni utaratibu wa utaalam wa kukadiria na kushauri kuhusu thamani ya mali isiyohamishika (kama vile ardhi,majengo na mazao). Hivyo neno uthamini linatokana na neno thamani

2.Thamani ni nini?

Thamani kwa ujumla wake inaweza kuelezeka kama bei inayolipwa kwa ajili ya kupata kitu. Lakini kwa lugha ya kitaaluma: thamani hususan ya mali isiyohamishika kwa mfano ardhi, inahusisha;-

  • Upatikanaji wake(availability)
  • Ubora wa matumizi yake(utility)
  • Mahali ilipo(location)
  • Umiliki wake(ownership)

3.Je, Ardhi ina thamani?

Ndiyo, kwa sababu ardhi ni rasilimali ya msingi ambayo shughuli zote za kijamiii, kiuchumi na kimaendeleo zinafanyika juu yake. Kwa Tanzania, asilimia takriban themanini (80) ya wananchi wa vijijini hutegemea ardhi kwa maisha yao ya kila siku kwa chakula, kipato na mahitaji mengine.

  • Ardhi ni rasilimnali adimu ambayo hushindaniwa na watu au shughuli mbalimbali na hivyo kuifanya iwe na thamani kubwa

· Ardhi humilikiwa kiserikali na kimila kwa sheria, kanuni na taratibu zinazokubalika. Ni kutokana na thamani ya ardhi watu hulazimika kumiliki ardhi na kuishi ndani yake.

4.Nini umuhimu wa uthamini?

Kuongezeka kwa ushindani wa mahitaji ya ardhi inayomilikiwa kiserikali, ikilinganishwa na ardhi iliyopo kumejenga umuhimu wa kusimamia na kutawala mali hiyo adimu kwa umakini mkubwa. Hivyo, uthamini ni nguzo mojawapo ya utawala na usimamizi bora wa ardhi kwa kuwezesha maamuzi ya maendeleo bora ya ardhi kufanyika.

5. Nini sababu ya uthamini?

Uthamini unaweza kutakiwa kwa madhumuni mbalimbali kama vile:

  • Ushauri wa maamuzi ya uuzaji na ununuzi
  • Kupandisha/kushauri bei ya pango
  • Rehani/mikopo
  • Bima
  • Ukadiriaji wa misingi ya utozaji kodi, ushuru na ada mbalimbali za kiserikali na uchumi
  • Sababu za kiuhasibu na mizani
  • Ukadiriaji fidia kutokana na utwaaji ardhi

6.Uthamini kwa madhumuni ya fidia:

Dhana ya fidia:

Kwa kuwa ardhi ya Tanzania ni mali ya wananchi wote, Rais ndiye mwenye dhamana ya kulinda kwa manufaa ya wote. Hata hivyo mwananchi anaruhusiwa kuitumia na pale ambapo inahitajika kutwaliwa kwa ajili ya sababu nyingine hasa za maendeleo ya taifa, basi mmiliki wa ardhi hiyo anastahili kulipwa fidia.

7. Nini misingi ya uthamini wa fidia?

  • Uthamini na ulipwaji wa fidia hufanyika kulingana na misingi ya taaluma na kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999(kifungu namba 3(I)(g) na kanuni zake husika).
  • Misingi ya uthamini wa fidia inatawaliwa na agizo la sheria ya uthamini wa haki, kamilifu na kulipwa kwa wakati muafaka (fair, full and prompt compensation)
  • kulingana na kifungu cha 3 cha Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na kanuni (taarifa ya Serikali Na.78 ya 2001) za fidia inapaswa ijumuishe yafuatayo pale panapohusika

· Thamani ya ardhi na mali isiyohamishika (unexhausted improvements)

  • Posho ya usumbufu (distabance allowance)
  • Posho ya usafiri (transport allowance)
  • Posho ya upotevu wa makazi (lost of accomodation)
  • Posho ya upotevu wa faida (loss of profit)
  • Gharama za awali za kupata ardhi
  • Kama fidia imecheleweshwa, ilipwe pamoja na riba kwa kiwango cha soko huria.

8.Taratibu za uthamini wa fidia

Uthamini hutekelezwa katika hatua kuu nne:

(a) Maandalizi ya awali (pre-site inspection):

  • Mthamini atatembelea eneo husika, ili kubaini ukubwa wa kazi na wahusika
  • Maandalizi ya vitendea kazi na viwango vya thamani.

b) Ukaguzi wa mali

  • Kumtambua mwenye mali na kumuorodhesha katika fomu ya ukaguzi
  • Kutoa namba ya kumbukumbu kwa mwenye mali
  • Mwenye shamba kuonyesha mipaka ya shamba au mali yake.
  • Kuchukua taarifa ya ukubwa wa eneo husika kwa kutumia GPS au ramani ya picha za anga

· Kuhesabu mazao ili kubaini idadi na kiwango cha ukuaji wa mazao ya aina mbalimbali

  • Kukagua majengo na kuchukua taarifa zote husika ikiwa ni pamoja na vipimo.
  • Kujaza taarifa ya majengo au idadi ya mazao kwenye fomu ya ukaguzi
  • Kumpiga picha mfidiwa mbele ya mali yake akiwa ameshika bango lenye namba ya kumbukumbu iliyotolewa
  • Kuhakikisha fomu ya ukaguzi imesainiwa na mwenye mali, Mthamini husika na Kiongozi wa Serikali ya Mtaa ambaye atathibitisha uhalali wa mfidiwa

) Ukokotoaji wa thamani

  • Taarifa huhamishwa kutoka fomu ya ukaguzi na kuingiza kwenye fomu ya ukokotoaji thamani
  • Ukokotoaji wa mahesabu ya thamani hutumia viwango vilivyotolewa na Ofisi ya Mthamini Mkuu ili kupata thamani ya mali husika
  • Kuwasilisha fomu zote kwa Mthamini kwa ajili ya kuthibishwa

d) Utayarishaji wa Hati za Fidia (Compensation Schedules)

Baada ya kumalizika uthamini na kuandaa taarifa,majedwali ya fidia yanatayarishwa yakionesha;

  • Majina ya walipwaji
  • Mali zitakazolipwa fidia
  • Thamani ya fidia kwa kila mali
  • Kisha jumla ya fidia itasainiwa na

1. Mthamini Mkuu

2. Afisa Ardhi anayeshughulika na zoezi hilo

3. Katibu Kata wa Kata husika

4. Mkuu wa Wilaya husika

5. Mkuu wa Mkoa

Ulipaji wa Fidia

Husimamiwa na Katibu Mtendaji kwa kuwatambulisha walipwaji fidia.

9.TARATIBU ZA UTHAMINI KWA UJUMLA ;

Kwa mwananchi anayehitaji huduma ya uthamini kuna taratibu za utendaji zinazohusisha:-

  • Maombi ya uthamini kwa maandishi yakiambatanishwa na kivuli cha hati au barua ya toleo

· Ili kumwezesha Mthamini aifanye kazi yake kwa ufanisi mkubwa, ushirikiano kati ya mteja na Mthamini unahitajika sana. Mteja anapaswa kuwa mwaminifu kwa kujibu maswali mbalimbali atakayoulizwa na Mthamini.

  • Mthamini hutakiwa kufanya ukaguzi wa mali (Physical site inspection)
  • Kisha ukokotoaji wa thamani hufanyika kwa kuzingatia viwango na kanuni za kitaalamu na za kisheria na hatimaye taarifa ya uthamini huandaliwa
  • Mteja hutakiwa kulipia ada ya uthamini kabla ya taarifa ya uthamini kuthibitishwa
  • Mwisho, taarifa ya uthamini huthibitishwa na Mthamini Mkuu na kisha kukabidhiwa kwa mwombaji.