Habari

ZINGATIENI UTU WAKATI WA KUWAHUDUMIA WANANCHI - DKT AKWILAPO

  • 27 Nov, 2025
ZINGATIENI UTU WAKATI WA KUWAHUDUMIA WANANCHI - DKT AKWILAPO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanazingatia utu wakati wa kuwahudumia wanachi.

 

Aidha, amewataka watumishi hao Kufanya kazi kwa umakini, uadilifu pamoja na kuzingatia miongozo ya utumishi wa umma wakati wote wa kutekeleza majukumu yao.

 

Mhe. Dkt Akwilapo amesema hayo leo tarehe 27 Novemba 2025 wakati alipotembelea Kliniki ya Ardhi inayoendeshwa katika mtaa wa Mbae Mashariki na Likombe katika Halmashuari ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

 

Amesema, dhamira ya wizara yake ni kutoa huduma bora na kwa wakati zenye nia ya kumaliza migogoro yote ya ardhi sambamba na kuagalia chanzo cha migogoro hiyo. 

 

"Falasafa ya Mhe Rais ni kuwaacha wananchi kuwa na furaha kwa kuondoa migogoro ya ardhi". amesema 

 

Amewataka wananchi wa Mtwara kuhakikisha wanamilikishwa maeneo yao kwa kupata hati milki za ardhi pamoja na kuwa na vibali vya ujenzi wanapotaka kuendeleza maeneo yao ili kuepuka migogoro.

 

Mhe. Dkt. Akwilapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kuitumia wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi.

 

Kwa upande wake kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara Bw. Fredrick Mrema amemueleza Waziri wa Ardhi kuwa, katika zoezi la Kliniki ya ardhi linaloendelea katika halmashauri ya Mtwara Mikindani takriban hati milki za ardhi 503 zimetolewa kwa wananchi wa mitaa ya Mbae na Likombe.

 

"Zoezi hili la kliniki ya ardhi ni endelevu na lengo letu tumepanga kuhudumia wananchi 10,984 katika kata nne za halmashauri hii ya mtwara mikindani" amesema Bw. Mrema.

 

Naye mkuu wa wilaya ya Mtwara Bw. Abdallah Mwaipaya aliyemuwakilisha mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amewahimiza wananchi wa wilaya yake kuhakikisha wanamiliki maeneo yao kwa kupatiwa hati milki za ardhi.

 

" Ndugu wananchi nawaombeni mmiliki maeneo yenu kwa kuwa na hati milki, hati ya ardhi inakupa uhakika wa milki na kilichofanywa na wizara katika kliniki hii ya ardhi kuwapatia wananchi hati ni jambo kubwa na ka kihistoria na niishukuru wizara ya ardhi" amesema.