Habari

ZAIDI YA MAOMBI 116 YAPITISHWA KWA WAWEKEZAJI WA MAENEO MBALIMBALI NCHINI

  • 05 Dec, 2025
ZAIDI YA MAOMBI 116 YAPITISHWA KWA WAWEKEZAJI WA MAENEO MBALIMBALI NCHINI

Kamati ya Kitaifa ya Kugawa Ardhi nchini imepitisha zaidi ya Maombi 116 kwa ajili ya wawekezaji kwenye Maeneo mbalimbali nchini likiwemo eneo na mradi wa uwanja AFCON unaojengwa mkoani Arusha.

 

Vibali hivyo vimeombwa kwa ajili ya madhumuni ya kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo viwanda,ufugaji pamoja na kilimo.

 

Kamati ya Kitaifa ya Kugawa Ardhi tarehe 3 Desemba imefanya ziara ya kikazi mkoani Arusha yenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ikiwemo eneo la mradi wa AFCON linalokadiriwa kuwa na ekari 4,570. 

 

Ziara hiyo imehusisha kufanyika kwa kikao cha 57 cha Kamati ya Kitaifa ya Kugawa Ardhi pamoja na kutembelea miradi inayosimamiwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA).

 

Akitoa taarifa kwa kamati, Afisa Mipango Miji Mkoa wa Arusha na Msimamizi wa Mradi wa AFCON, Bi.Georgia Mwambegele alisema, mradi huo unaoendelea jijini Arusha unajumuisha maeneo mbalimbali ikiwemo ekari 83 zilizotengwa kwa ajili ya uwanja wa mpira pamoja na ekari 208 za Mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi (KKK) ambao tayari umetoa jumla ya viwanja 469.

 

Kwa upande wake, Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Arusha Bw. Frank Minzikunte alisema, Serikali imetoa maelekezo ya kuchukua ekari 370 kwa ajili ya uwekezaji, sambamba na kuridhia utekelezaji wa upimaji shirikishi kwa wananchi.

 

Alibainisha kuwa, tayari shilingi bilioni 20 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi, upangaji na upimaji wa maeneo hayo.

 

Kwa mujibu wa Minzikunte, baada ya mashindano ya AFCON 2027, maeneo hayo yataendelezwa ili yaendelee kutoa huduma za kiuchumi kupitia viwanda, biashara, barabara na miradi mingine ya halmashauri kwa manufaa ya wananchi.

 

Kamati ya Kugawa Ardhi ina jukumu la kumshauri Kamishna wa Ardhi nchini katika kuamua kuhusu maombi ya haki ya kumiliki ardhi.