Habari
WIZARA YA ARDHI YAPATIWA MAFUNZO YA MATUMIZI YA MFUMO WA e-MREJESHO
- 15 May, 2026
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na taasisi zake imepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya Mfumo wa e-Mrejesho yanayotolewa na wataalamu kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mafunzo hayo ya siku tatu (3) yana lengo la kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza Mei 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dodoma, mwezeshaji kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Hassan Kilenza, amesema mafunzo hayo ya mfumo wa e-mrejesho yanalenga kuwapa wananchi fursa ya kutoa maoni, mapendekezo, pongezi na malalamiko kuhusu huduma wanazopata kutoka katika Sekta husika.
Aidha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala kutoka Wizara ya Ardhi, Bw. Deodatus Mwiliko amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa kushughulikia kero za wananchi, ambapo amesema kupitia mfumo huo taarifa zitapokelewa, kufanyiwa kazi na wananchi watapatiwa mrejesho kwa wakati.
Mfumo wa e-Mrejesho ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kusikilizwa na changamoto zake kushughulikiwa kwa wakati, popote alipo.
Mfumo huo unapatikana kwa njia mbalimbali kama kupitia tovuti emrejesho.gov.go.tz, au unaweza kupakua app ya e-Mrejesho kupitia App Store au Google Play Store au kupitia *152*00# baada ya hapo unafuata maelekezo.