Habari

WAZIRI NDEJEMBI ATOA SIKU TATU UHAKIKI WA MPAKA ENEO LENYE MGOGORO KIMBIJI

  • 18 Jul, 2025
WAZIRI NDEJEMBI ATOA SIKU TATU UHAKIKI WA MPAKA ENEO LENYE MGOGORO KIMBIJI

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi ameielekeza Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam mpaka kufikia Jumatatu ya Julai 21, 2025 iwe imewasilisha taarifa ya kurejesha mipaka ya kiasili ya eneo linalolalamikiwa lililopo Kimbiji katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo Julai 18, 2025 alipotembelea eneo hilo na kufanya kikao cha pamoja na pande zenye mgogoro.

“ Naielekeza Ofisi ya Kamishna kurejesha mara moja mipaka ya kiasili ya eneo hili na kuwasilisha taarifa ofisini kwangu Julai 21, 2025 ili tumalize mgogoro huu wa muda mrefu.

Rai yangu kubwa kwa watanzania pale wanapoenda kuuziana ardhi wahakikishe wanapata vipimo halisi vya eneo husika na washirikishe mamlaka za ardhi ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kwenye siku za usoni,” Amesema Mhe. Ndejembi.

Mgogoro huo unahusisha Familia ya Jokoo na Bi. Lilian Kileo ambapo mmoja wa wanafamilia (Omary Hamis Ally ) ambaye anatajwa kumuuzia Bi. Kileo eneo lake pamoja na sehemu ya eneo linalodaiwa kuwa ni la Familia ya Jokoo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Ndejembi ameambatana na Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukrani Kyando pamoja na wataalamu wa wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni.