Habari

WAWEKEZAJI WA MASHAMBA ARUSHA WAMPONGEZA WAZIRI SILAA

  • 15 Jan, 2024
WAWEKEZAJI WA MASHAMBA ARUSHA WAMPONGEZA WAZIRI SILAA

Wawekezaji wa Mashamba wa jiji la Arusha wametoa shukran zao za dhati kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa kwa kukutana nao kwa mara ya kwanza jambo ambalo halijawakutokea hapo kabla.


Waziri Silaa amekutana na Wawekezaji hao kwa lengo la kuwapa maelekezo ya Serikali kuhusu umiliki wa mashamba na suluhu ya uvamizi wa mashamba ya watu wenye hati unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.


Wawekezaji hao wa mashamba wametoa shukurani zao na wengine kustaajabu kitendo cha Waziri wa Ardhi kukutana nao jijini Arusha na kuwasikiliza changamoto zao, jambo ambali halijawahi kutokea hapo kabla.


Katika kikao hicho Waziri Silaa amepiga marufuku kwa wananchi  kuvamia ardhi za watu wengine waliona hati na kuwataka Viongozi waache kuhamasisha wananchi kuvamia maeneo ya watu.


Silaa amewaeleza wawekezaji hao na watumishi wa sekta ya ardhi waliokuwepo kuwa Wataalam wa Sekta ya Ardhi watekeleze Mpango Kabambe wa Jiji la Arusha kwa vitendo badala ya maneno.


Pia, Watendaji wote wa Sekta ya Ardhi wafanye kazi bila kuwabugudhi wamiliki halali wa ardhi, wafanye kazi kwa kusikiliza wananchi wanaohitaji huduma kutoka katika ofisi zao na haki ya umiliki iheshimiwe.


Aidha, amesisitiza kuwa ni wajibu wa wamiliki wa ardhi kufuata masharti ya umiliki wa ardhi kwa kuyaendeleza na Maeneo yote ya mashamba ya mjini yasanifiwe na iandaliwe taarifa ya mashamba yaliyopimwa kinyume na utaratibu wa vikao vya wamiliki.


Ameongeza pia, Wataalam wote wa ardhi wanaoandaa mapendekezo ya kufuta umiliki ardhi kwa sababu zisizokuwa sahihi waache mara moja, na katika kutekeleza hili atatuma Timu ya Waziri ya kuhakiki malalamiko ya ufutaji ili Kamishna wa Ardhi aone kama mapendekezo hayo yalikuwa sahihi.