Habari
WATUMISHI WAPYA 225 WIZARA YA ARDHI WAFUNDWA KUHUSU UTUMISHI WA UMMA
- 13 Feb, 2026
Jumla ya watumishi wapya 225 wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutoka fani mbalimbali wamehitimisha mafunzo elekezi yaliyolenga kuwaandaa rasmi kwa majukumu yao ndani ya utumishi wa umma.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo tarehe 12 Februari 2026, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Mhandisi Anthony D. Sanga, amesisitiza umuhimu wa watumishi hao kuzingatia miiko ya utumishi wa umma, kutunza siri za Serikali, kufuata sheria, taratibu na kanuni, pamoja na kuwahudumia wananchi kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji.
Mhandisi Sanga amewakaribisha rasmi watumishi hao ndani ya Wizara na kuwaasa kufuata maelekezo ya viongozi wao, kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na heshima ili kuchangia kikamilifu katika kufanikisha malengo ya Wizara na Serikali kwa ujumla.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa ajira 400 katika Wizara ya Ardhi, akieleza kuwa hatua hiyo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali katika kuimarisha rasilimali watu na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kupitia mafunzo hayo, watumishi wapya wamejengewa uelewa mpana kuhusu maadili ya kazi, wajibu wa mtumishi wa umma, utunzaji wa taarifa za Serikali, pamoja na namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.