Habari
WATUMISHI ARDHI WATAKIWA KUTOKUA SEHEMU YA MIGOGORO YA ARDHI
- 01 Oct, 2025

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga, amewataka watumishi wa Wizara hiyo kutojihusisha na migogoro ya ardhi, na badala yake wawe sehemu ya suluhisho kwa kutoa huduma bora na kwa wakati.
Akizungumza katika kikao kazi cha watumishi wa Wizara hiyo Makao Makuu kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara Mtumba, jijini Dodoma, Mhandisi Sanga amesema kuwa, kipaumbele cha Wizara ni kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kupatiwa suluhisho la haraka katika changamoto mbalimbali zinazohusu sekta ya ardhi.
Aidha, amewataka watumishi hao kutozoea matatizo na wachukue hatua za haraka katika kushughulikia changamoto za ardhi.
"Kila tatizo linalowasilishwa na mwananchi ni dharura. Watumishi mnatakiwa kuchukua hatua za haraka na kuhakikisha mnatatua changamoto hizo kwa ufanisi," alisema Mhandisi Sanga.
Amesisitiza umuhimu wa kusikiliza kero za wananchi kwa wakati huku akionya watumishi wa sekta ya ardhi kutokuwa sehemu ya kero hizo kwa kuchelewesha kutoa huduma au kutoa ahadi zisizotekelezeka.
"Wananchi lazima wasikilizwe kwa wakati. Tuwahudumie kwa ufanisi na tusiwe sehemu ya changamoto kwao. Hili ndilo jukumu letu la msingi," aliongeza.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Ardhi, Bw. Hussein amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuwa mabalozi wa utatuzi wa migogoro hiyo katika maeneo yao ya kazi.
"Ni muhimu kila mtumishi kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma bora. Epukeni kutoa ahadi zisizotekelezeka kwa wananchi kwani ndicho chanzo kikubwa cha migogoro mingi," alisema Bw. Hussein.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi, Bw. Deogratius Kalimenze, amewahimiza watumishi wa sekta ya ardhi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kutumia lugha nzuri pale wanapowahudumia wananchi.
"Tutumie lugha ya staha, tuwe waadilifu na tuwaheshimu wananchi katika mahitaji yao ya huduma. Hii itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi isiyo ya lazima," alisema Bw. Kalimenze.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imejipanga kuboresha huduma za sekta ya ardhi kwa kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.