Habari

WANANCHI MOROGORO WAHAMASISHWA KUTUMIA FURSA YA HUDUMA ZA ARDHI KATIKA TAMASHA LA UTAMADUNI

  • 26 Aug, 2026
WANANCHI MOROGORO WAHAMASISHWA KUTUMIA FURSA YA HUDUMA ZA ARDHI KATIKA TAMASHA LA UTAMADUNI

Wananchi mkoani Morogoro wamehamasishwa kufika kwa wingi katika Banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi lililopo katika Uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro, ili kupata huduma mbalimbali za ardhi pamoja na elimu kuhusu masuala ya umiliki na matumizi bora ya ardhi.

 

Wito huo umetolewa Agosti 25, 2026, na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro, Bw. Idrissa Kayera wakati wa Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linaloendelea mkoani humo.

 

Bw. Kayera amesema ushiriki wa Wizara katika tamasha hilo ni fursa muhimu kwa wananchi kupata huduma za ardhi kwa urahisi, haraka na kwa wakati, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata huduma  mbalimbali za sekta ya Ardhi ikiwemo umiliki wa ardhi.

 

Amesema wananchi wanakaribishwa katika banda hilo na kupata elimu kuhusu taratibu za umiliki wa ardhi, hati za miliki pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na Wizara, hivyo kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na ukosefu wa uelewa kuhusu masuala ya ardhi.

 

“Tunawahamasisha wananchi wa Morogoro na maeneo ya jirani kufika kwa wingi katika banda la Wizara ya Ardhi ili kupata huduma mbalimbali na elimu kuhusu masuala ya ardhi. Hii ni fursa muhimu ya utapata huduma kwa haraka na kwa wakati,” amesema Bw. Kayera.

 

Aidha, amesema katika tamasha hilo, waataalamu wa Wizara watatoa pia hati za kimila ikiwa ni sehemu ya kudumisha utamaduni na mila za watanzania katika masuala ya ardhi.

 

Tamasha hilo la Nne la Kitaifa la Utamaduni linafanyika mkoni Morogoro kuanzia Agosti 25 hadi 29, 2026, katika Uwanja wa Jamhuri, likiwa na kaulimbiu: “Utamaduni Wetu, Nguzo ya Maadili, Uchumi Jumuishi na Utaifa karibu AFCON 2027.”