Habari

WANANCHI 594 WAKABIDHIWA HATI MILIKI KATIKA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

  • 13 Oct, 2025
WANANCHI 594 WAKABIDHIWA HATI MILIKI KATIKA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Wananchi 594 wamekabidhiwa hati miliki za ardhi katika mkoa wa Njombe, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja katika sekta ya ardhi.

 

Huduma hiyo inatolewa kupitia Kliniki za Ardhi zinazoendelea katika kata za Matembwe, Kifanya, Makete na Ilangamoto wilayani Njombe mkoa wa Njombe.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 10, 2025, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Njombe, Fulgence Kanuti, amesema zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanamiliki ardhi kihalali na kupata nyaraka rasmi.

 

“Katika maeneo yote manne, jumla ya viwanja takribani 4,800 vimepimwa kupitia mazoezi ya urasimishaji yaliyofanyika kwa ushirikiano kati ya ofisi ya ardhi mkoa wa Njombe, halmashauri ya Mji na Wilaya ya Njombe pamoja na sekta binafsi za upangaji na upimaji,” alisema Kanuti.

 

“Matarajio yetu ni kuwafikia wananchi wote hawa 4,800 ambao maeneo yao tayari yamepimwa, ili kuwamilikishia na kuwapatia hati miliki za ardhi zitakazowasaidia kiuchumi,” aliongeza Kanuti.

 

Kwa mujibu wa Kanuti, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na kampuni binafsi imeendelea kurasimisha maeneo ya wananchi kwa mujibu wa sheria, huku huduma ya kutoa elimu ya ardhi ikiendelea kutolewa kwa wananchi wote waliotembelea kliniki hizo.

 

“Migogoro mingi ya ardhi Njombe ni midogo midogo na inasababishwa zaidi na ukosefu wa uelewa. Kupitia elimu tunayotoa katika kliniki hizi, migogoro mingi imekuwa ikitatuliwa mara moja,” amesema.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Saleko, amesema ameridhishwa na mwamko mkubwa wa wananchi wa Njombe kushiriki katika zoezi hilo la urasimishaji.

 

“Wananchi wengi wamejitokeza kufuata huduma za upimaji na usajili wa hati. Wale waliokuwa tayari wamelipia na kujaza nyaraka walipatiwa hati zao papo hapo,” alisema Saleko.

 

Baadhi ya wananchi walionufaika na zoezi hilo wameeleza furaha yao kwa Serikali kuwapelekea huduma hizo karibu. Riziki Nisilu, mkazi wa Njombe, amesema huduma hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao.

 

“Tunashukuru kwa huduma hii ya urasimishaji wa ardhi. Kupata hati miliki kutatuwezesha kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha na kukuza uchumi wetu,” alisema.

 

Huduma katika klinik ya ardhi zinaendelea kutolewa katika mkoa wa Njombe mpaka tarehe 17 Oktoba 2025 ikiwa ni juhudi za Wizara ya Ardhi kuhakikisha inawafikia wananchi wengi kwa kuwapatia huduma mbalimbali za sekta ya ardhi.