Habari

WADAU SEKTA YA MILKI WAFUNDWA WATAKIWA KUWA WAADILIFU 

  • 05 Dec, 2025
WADAU SEKTA YA MILKI WAFUNDWA WATAKIWA KUWA WAADILIFU 

Wadau wa sekta ya milki nchini wametakiwa kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao ili kujenga uaminifu kwa wateja wanaowahudumia.

 

Akizungumza mapema leo Desemba 03, 2025 katika kikao kilichowakutanisha Wataalam wa Ardhi, Mawakala wa Milki, Wamiliki wa Makazi na watoa huduma mbalimbali katika sekta ya milki katika Ukumbi wa Top Life Mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Upendo Matotola amesema, kumekuwa na Chembechembe za kukosa Uadilifu na uwajibikaji kwa baadhi ya wadau wa sekta ya milki jambo alilolieleza kwamba linapoteza imani kwa jamii.

 

"Tukiwa waadilifu na tukawa tunawajibika basi hizi Kazi tutazipata kwa wingi zaidi" amesema Dkt. Matotola

 

Aidha, Dkt. Matotola ameweka wazi kuwa, Wakala wa Milki nchini ni kiungo muhimu katika kutimiza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya Serikali kushirikiana na Sekta binafsi 

 

"Soko la Milki mmelibeba kwa hiyo tunapokaa kushirikiana na nyie ni kwa sababu ni wadau muhimu sana kwenye soko lakini pia tunatimiza azma ya Mhe. Rais ya Kushirikiana na Sekta binafsi". Ameongeza Dkt Matotola

 

Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Bw. Idrissa Kayera amewataka wadau wa sekta ya milki kutumia njia za kisasa za kidigitali ikiwemo mitandao ya kijamii kutangaza fursa mbalimbali za Uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Milki.

 

" Tufikirie kwa uwanda mpana sana katika kuwavutia wawekezaji kuliko hali ya sasa hivi" amesema Kayera

 

Kwa upande wao, washiriki wameishukuru Wizara ya Ardhi kwa kuandaa Mkutano huo na kuendelea kutoa elimu waliyoieleza kuwa, inawasaidia kuboresha utendaji kazi wao na kupunguza migongano isiyo ya lazima. 

 

Wamesema, mafunzo hayo yanachochea uwajibikaji, weledi na ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.

 

"Sisi kwa upande wetu tupo tayari kabisa kushirikiana na nyie mkituhitaji muda wowote" amesema David Isote Katibu wa Madalali.

 

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Kitengo cha Milki (Real Estate) inaendesha mijadala ya pamoja na wadau kwa lengo la kupata maoni kuhusu utambuzi na usajili wa Wadau wa Sekta ya Milki ili kuboresha na kukuza sekta ya milki nchini.

 

Mijadala hiyo inalenga kutoa elimu, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya milki nchini ambapo tayari kitengo hicho kimefanya vikao vya mijadala katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha Dodoma, Mwanza na Sasa Mkoa wa Morogoro.