Habari
SERIKALI YAWATAKA WATHAMINI KUEPUKA KUFANYA KAZI KWA MASLAHI BINAFSI
- 05 Dec, 2025
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amewataka Wathamini nchini kuepuka kufanya kazi kwa maslahi binafsi na badala yake wafanye kazi kwa maslahi ya Umma huku wakizingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya Sekta hiyo.
Mhe. Mmuya ameyasema hayo tarehe 05 Desemba 2025 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Sita wa Wathamini kwa niaba ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo uliofanyika mkoani Morogoro.
Aidha, Mhe. Mmuya amewasisitizia Wathamini hao kuepuka kufanya kazi kwa kusukumwa na maslahi binafsi wakati wote wa kutekeleza majukumu yao
"Tumieni weledi, tumieni maarifa yenu mtoe taarifa halisi ili zilete muafaka wa jambo mnalofanya kwa faida ya mteja wako na hata kwa mlaji anayepelekewa tenda ili kuepuka kufanya kazi kwa kusukumwa na maslahi binafsi" amesema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.
Kadhalika Mhe. Mmuya amewaasa Wathamini kutenda haki pale wanapotekeleza majukumu yao ikiwa ni kutafsiri kwa vitendo dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufanya kazi kwa kuzingatia utu.
"Tutende haki kwa watu wetu tunaowasimamia na kama hufanyi vema kwa wale unaowasimamia thamani yako wewe kwao iko wapi" amesisitiza Mhe. Mmuya.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kaspar Mmuya ameiomba bodi ya Usajili wa Wathamini kufanya kazi kwa kutumia mifumo ili kurahisisha utendaji kazi na kuongeza uhalisia katika matokeo ya shughuli za uthamini.
"Naombeni sana, tumieni mifumo kwa kazi zetu angalau asilimia 80 hadi 90 kwani inaturahisishia kazi, inaongeza uwazi na inapunguza gharama".
Mkutano Mkuu wa sita wa Wathamini umefanyika kwa siku mbili kuanzia Desemba 04 hadi 05,2025 ukiongozwa na kaulimbiu inayosema "Taaluma ya Uthamini katika nyakati za mabadiliko ya kiteknolojia"
Kaulimbiu hiyo imelenga kutoa elimu, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo muhimu katika uchumi wa nchi.