Habari

SERIKALI YARIDHISHWA NA KAZI YA UTHAMINI ENEO LA MRADI WA SGR KIGOMA 

  • 20 Dec, 2025
SERIKALI YARIDHISHWA NA KAZI YA UTHAMINI ENEO LA MRADI WA SGR KIGOMA 

Mthamini Mkuu Msaidizi anayeshughulikia uthamini wa jumla Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Chiremeji Kome ametembelea na kukagua eneo linalofanyiwa uthamini kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) lenye urefu wa kilomita 5 kutoka Katosho hadi Kigoma Mjini, ikiwa ni sehemu ya mradi mkubwa wa reli kutoka Tabora hadi Kigoma.

 

Akiwa katika eneo hilo tarehe 17 Desemba 2025 mkoani Kigoma Bw. Chiremeji amekutana na timu ya wataalamu inayotekeleza kazi hiyo ambapo alionesha kuridhishwa na kazi inayofanywa na timu hiyo.

 

Akizungumza na wataalamu hao wakati wa ziara yake amewataka kufanya kazi kwa weledi huku wakihakikisha kuwa, hawazalishi migogoro wakati wa kutekeleza majukumu yao.

 

Amewaambia wataaalamu hao kufanya kazi kwa kasi kwa kuwa eneo linalofanyiwa uthamini linahitajika haraka kwa ajili ya kukabidhiwa kwa mkandarasi.

 

Aidha,Bw. Chiremeji ameipongeza timu ya wataalamu wa uthamini kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwaeleza kuwa, serikali inafuatilia kwa karibu kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati. 

 

"Macho na masikio ya Serikali yako kwenye mradi huu. Tunawategemea sana, hivyo hakikisheni kila mwananchi anapata haki yake kwa wakati. Fanyeni kazi kwa umakini na weledi,” alisema Bw. Chiremeji.

 

Kwa mujibu wa Bw. Chiremeji, ni muhimu kwa watendaji kuwa na lugha na kauli njema wanapotoa huduma kwa wananchi, kwani ni sehemu ya kuwaheshimu na kuwahudumia kwa staha.

 

Kiongozi wa timu ya uthamini, Bw. Rashid Mgetta, amemshukuru Bw. Chiremeji kwa ziara hiyo na kueleza kuwa, timu yao inatekeleza jukumu la uthamini wa fidia kwa kipande cha sita cha mradi wa SGR kutoka Tabora hadi Kigoma, wenye jumla ya kilomita 412.

 

Kwa niaba ya wapima ardhi, Bw. Oscar Mwanzalila alieleza kufarijika kwao kutembelewa na viongozi waandamizi na kueleza kuwa,  uongozi huo unawapa ari ya kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii na uadilifu.

 

Zoezi la uthamini linaendelea katika wilaya sita zinazopitiwa na mradi huo, ambazo ni Tabora Mjini, Uyui, Urambo, Kaliua, Uvinza na Kigoma. Taarifa za mali za wananchi zinakusanywa kwa ufanisi ili kuwezesha ulipaji wa fidia stahiki kwa wakati.

 

Mradi wa huu unatekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), ambapo Ofisi ya Mthamini Mkuu , wizara ya Ardhi imepewa jukumu la kufanya uthamini wa fidia kwa vipande vya pili hadi sita vya mradi huo mkubwa wa kimkakati. Kwa sasa, kazi inaendelea katika kipande cha sita.