Habari
SERIKALI YAAGIZA KUKAMILISHWA KWA MCHAKATO WA HATI YA KIWANJA CHAMWINO
- 12 Mar, 2026
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya, ametoa maelekezo kwa wataalamu wa ardhi katika Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanamkabidhi hati miliki ya Kiwanja Na. 104, Block B Chamwino, Bi. Mary Vicent Mbulula, mkazi wa Mtaa wa Nduka, kabla ya mwisho wa saa za kazi leo.
Maelekezo hayo yametolewa leo, tarehe 11 Machi 2026, kufuatia ziara ya Naibu Waziri huyo nyumbani kwa mwananchi huyo kwa lengo la kujionea hali halisi na kubaini sababu zilizokuwa zikikwamisha mchakato wa kupatiwa hati miliki ya kiwanja hicho licha ya kukamilisha taratibu zinazohitajika.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri Mmuya alisisitiza umuhimu wa kushughulikia kwa wakati changamoto zinazowakabili wananchi, hususan pale ambapo taratibu zote za kisheria zimekamilika.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma, Godfrey Mwamsojo, amesema ofisi yake itatekeleza maelekezo hayo na kuhakikisha mwananchi huyo anakabidhiwa hati miliki yake kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa.
Aidha, Naibu Waziri Mmuya amewasisitiza watumishi wa umma kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi, uwazi na kwa wakati, akibainisha kuwa Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za ardhi ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati.