Habari
SERIKALI KUJENGA KANZIDATA KUU YA TAARIFA ZA ARDHI
- 09 Sep, 2026
Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya Taarifa za Kijiografia za Ardhi Nchini (National Land Data Infrastructure - NLDI) unaolenga kujenga kanzidata kuu ya kitaifa ya taarifa za ardhi ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi, za kisasa na zinazotambulika rasmi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati alipotembelea Ofisi za Mradi wa NLDI jijini Dodoma kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.
Amesema kanzidata hiyo itakuwa kitovu cha taarifa mbalimbali za msingi kuhusu ardhi na kuwezesha wadau kupata taarifa za kijiografia kwa matumizi mbalimbali kupitia jukwaa maalum litakalojengwa chini ya mradi huo.
“Wizara ya Ardhi lazima iwe custodian wa taarifa za ardhi nchini. Tunataka kujenga miundombinu ya kitaifa itakayotuunganisha na kutupatia data sahihi za ardhi zitakazokuwa rejea kwa matumizi mbalimbali,” amesema.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha Tanzania kupata picha za kisasa za anga na taarifa sahihi za maeneo mbalimbali, tofauti na hali ya sasa ambapo baadhi ya taarifa zinazotumika zimepitwa na wakati.
Aidha, amesema mfumo huo utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi inayotokana na tafsiri tofauti za mipaka, mwingiliano wa matumizi ya ardhi na umiliki, kwa kuhakikisha taarifa rasmi zinapatikana kutoka katika mamlaka husika.
Naibu Waziri amewataka wataalamu wanaotekeleza mradi huo kutumia fursa hiyo kuhakikisha Tanzania inajenga mfumo imara utakaosaidia kulinda ardhi kisayansi na kidijitali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo ndege zisizo na rubani, katika ukusanyaji wa taarifa sahihi za ardhi ili kuimarisha mipango na usimamizi wa rasilimali ardhi nchini.