Habari

PINDA APIGA MARUFUKU WENYEVITI WA VIJIJI NA MITAA KUUZA MAENEO

  • 24 Oct, 2023
PINDA APIGA MARUFUKU WENYEVITI WA VIJIJI NA MITAA KUUZA MAENEO

Na. Hassan Mabuye, Simanjiro - Manyara

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Geophrey Pinda amepiga marufuku wenyeviti wa vijiji kuuza viwanja na mashamba kwa kuwa mamlaka hayo sio ya kwao kwani wanasababisha migogoro ya ardhi isiyo na tija.

Pinda amesema hayo wakati alipofanya ziara katika kijiji cha Kitwai B wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara ili kukutana na wananchi wenye mgogoro wa mpaka kati ya wilaya ya Kilindi mkoa wa Tanga na wilaya Simanjiro mkoa wa Manyara.

"Hakuna mgogoro wowote wa mipaka huku, tatizo liliopo hapa ni baadhi ya viongozi hususan wenyeviti wa vijiji kuuza maeneo kiholelaholela kwa watu wanao wajua wao. Na kuanzia leo ni marufuku uuzaji wa maeneo chini ya mamlaka ya wenyeviti wa vijiji sababu ndio chanzo kikubwa cha migogoro" Amesema Pinda.

Aidha, Pinda amemuomba Waziri wa TAMISEMI kumsimamisha mwenyekiti wa Kijiji cha Gitu wilaya Kilindi mkoani Tanga kwa kuwa ndio chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi ya eneo hilo kwani amekuwa akiuza ardhi bila kufuata taratibu za mipango ya matumizi ya ardhi.

Katika Hatua nyingine Pinda ameelekeza kuondolewa Mpima Ardhi Msaidizi wa mji wa Merelani Francis Sulle kwa kuwasumbua wananchi na kukaidi maelekezo ya viongozi wa Serikali katika kusimamia masuala ya upimaji na umilikishaji wa ardhi.

"Yule Afisa Ardhi wa Merelani anasumbua wananchi wa Merelani, huyu naondoka nae mimi kwenda nae Dodoma sababu ameshindwa kufanya kazi yake na amekuwa akikaidi maelekezo mbalimbali anayopewa na viongozi wake wa Serikali kuu na Wilaya" Alisema Pinda.

Pinda amesisitiza kuwa utaratibu wa umilikishaji wa ardhi za vijiji unawataja wakurugenzi wa Halmashauri ambao ndio wasimamizi wa utaratibu wa umilikishaji wa ardhi za vijiji na sio wenyeviti wa vijiji japo ardhi hiyo inamilikiwa na kijiji.

Kwa upande wa mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Kilindi na Simanjoro Naibu Waziri Pinda amesema hakuna mgogoro wowote wa wilaya hizo mbili bali ni baadhi ya viongozi wa vijiji kuuza maeneo yaliyowekewa mipango ya matumizi ya ardhi kiholela.

Pinda amewataka wakazi hao kuishi kwa amani na upendo bila kugombana na kuepuka ugomvi wa mipaka hadi hapo yatakapokuja maelekezo rasmi ya Serikali ya usimamizi wa eneo hilo.