Habari

PINDA AIWAKILISHA TANZANIA MKUTANO WA 44 SHELTER AFRIQUE ALGERIA

  • 18 Jul, 2025
PINDA AIWAKILISHA TANZANIA MKUTANO WA 44 SHELTER AFRIQUE ALGERIA

Algiers, Algeria – Julai 17, 2025

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geophrey Mizengo Pinda (Mb), ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano Mkuu wa 44 wa mwaka wa taasisi ya Shelter Afrique, unaoendelea jijini Algiers, Algeria kuanzia Julai 15 hadi 17, 2025.

Mkutano huo unalenga kujadili fursa za upatikanaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu kwa nchi 44 wanachama wa taasisi hiyo ya fedha ya maendeleo ya makazi barani Afrika.

Mhe. Pinda ameambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Dkt. Upendo Matotola, Mkurugenzi wa Kitengo cha Milki,
Bw. Awadhi Salim, Mkurugenzi Msaidizi wa Nyumba na Uendelezaji Milki, Bw. Richard Ndeona, Meneja wa Hazina kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Shelter Afrique ni taasisi ya Kimataifa iliyoanzishwa na nchi 44 wanachama kwa lengo la kuchochea maendeleo ya sekta ya makazi na miji Afrika. 

Tangu mwaka 2023, taasisi hiyo imeanza kufanya kazi kwa mfumo wa benki na sasa inajulikana kama 
Shelter Afrique Development Bank (ShafDB), ambapo Tanzania ni miongoni mwa wanahisa wake ambapo Makao Makuu ya benki hiyo yapo jijini Nairobi, Kenya.