Habari

NAIBU WAZIRI KASPAR MMUYA ATOA WITO WA KUDUMISHA AMANI

  • 28 Dec, 2025
NAIBU WAZIRI KASPAR MMUYA ATOA WITO WA KUDUMISHA AMANI

 

Ruangwa Lindi. 

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.  Kaspar Mmuya amewataka Watanzania kuendelea kuilinda amani ya nchi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, akibainisha kuwa, amani ndiyo nyenzo muhimu inayowezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na ustawi wa wananchi.

Mhe. Mmuya ametoa wito huo leo Desemba 26, 2025 wakati wa ibada ya kumbukizi ya baba yake mzazi marehemu Kaspar Selemani Mmuya, iliyofanyika Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Nanganga, Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.

Amesema kuwa, Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa Barani Afrika kutokana na misingi ya amani, umoja na utulivu iliyojengwa kwa miaka mingi, hali iliyoiwezesha Serikali kuendelea kuwahudumia wananchi na kusimamia maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo ardhi na makazi.

"Dkt . Samia Suluhu Hassan anatukumbusha tupendane sisi wenyewe kwa wenyewe na tuipende nchi yetu" amesema Naibu Waziri Kaspar Mmuya .

Katika tukio hilo, Mhe. Mmuya kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo  amewatakia Watanzania heri za Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya ambapo amewataka kusherehekea kwa amani upendo na Utulivu.

"Kwa niaba ya sekta ninayoisimamia ambayo Waziri wangu Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo anawatakia siku hii njema, tusheherehekee tukiwa na amani" amesema Naibu Waziri Kaspar Kaspar.

Aidha, Mhe. Mmuya ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusisitiza mshikamano wa kitaifa, maadili mema na kuheshimiana kama msingi wa kuijenga Tanzania yenye maendeleo endelevu na jumuishi.

"Sisi tubaki kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake" amesema Naibu Waziri Kaspar Mmuya.

Kadhalika, Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa wananchi kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwa imara zaidi katika kuliongoza taifa, hatua itakayoiwezesha Serikali kuendelea kusimamia amani, kuimarisha huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo yanayogusa maisha ya watu.