Habari

MZAVA: TUMERIDHIKA NA KAZI YA UPANGAJI MATUMIZI YA ARDHI 

  • 29 May, 2025
MZAVA: TUMERIDHIKA NA KAZI YA UPANGAJI MATUMIZI YA ARDHI 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na kazi ya upangaji matumizi ya ardhi katika Kijiji cha Msungua kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

 

Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho katika mkutano wa hadhara, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava amesema, kamati yake imeridhishwa na kazi ya upangaji matumizi katika kijiji cha Msungua ambapo anaamini kukamilika kwake kutawezesha wananchi kupata hati za maeneo yao.

 

“Sisi kama kamati, tumeridhika na kwa kazi nzuri inayofanywa, wananchi wanaijua hii ni kazi yao, wameshiriki vizuri. Tumeridhika na kasi ya kutekeleza kazi ya upangaji wa matumizi ya ardhi” amesema Mhe. Mzava.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Mhe. Geophrey Pinda amesema, utekelezaji wa kazi hiyo unasaidia wananchi kuondokana na migogoro ya mipaka ya vijiji, Jirani na Jirani katika maeneo yao na kuwataka kuheshimu mkakati na mipango waliojiwekea ya matumizi ya ardhi.

 

“Lindeni maeneo haya ili fedha za serikali zikiletwa kuwe na maeneo ya kutekeleza miradi ya maendeleo, maeneo yaliyopangwa kwa huduma za jamii mkayatunze na mkipata hati tambueni, hati ni mtaji zitasaidia kustawisha Maisha ya wananchi” amesema Naibu Waziri Pinda.

 

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi hiyo kwa Kamati kwa kamati ya Bunge mkoani Singida, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Bw. Joseph Mafuru ameeleza kuwa, hadi Mei 2025 jumla ya vijiji 224 sawa na asilimia 67.27 vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi katika halmashauri za wilaya 14 huku vijiji 109 kati ya 333 mipango yake ya matumizi ikitarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2025.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imefanya ziara mkoani Singida kwa lengo la kukagua utekelezaji wa kazi ya upangaji wa matumizi ya ardhi katika Kijiji cha Msungua, kazi inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.

 

Itakumbukwa Machi 2025 Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ilipokea fedha kiasi cha Sh. Bilioni tano kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 333 kikiwemo Kijiji cha Msungua.

 

Ili kukamilisha kazi hiyo kikamilifu Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wameitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kukamilisha kazi hiyo katika Kijiji cha Msungua kwa kuwapatia wananchi Hati za maeneo yao.