Habari
MMUYA AITAKA NHC LINDI KUKAMILISHA UJENZI WA MTANDA COMMERCIAL COMPLEX KUFIKIA JANUARI MOSI 2026
- 20 Dec, 2025
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Mmuya amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuongeza kasi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi yake ya kimkakati, ikiwemo Mradi wa Jengo la Kibiashara la Mtanda Commercial Complex linalokadiriwa kuwa na Thamani ya Bilioni 4.26
Akizungumza Mkoani Lindi wakati wa ziara yake Mhe. Mmuya amesema Shirika limepewa dhamana kubwa ya kuongoza na kuchochea maendeleo nchini, hivyo ni lazima lifanye kazi kwa weledi, ufanisi na kwa kasi inayolingana na matarajio ya Taifa.
Mhe. Mmuya Amesisitiza pia ni muhimu kwa Shirika hilo kutumia mitandao ya kijamii ili kutangaza fursa zake kuwavutia wawekezaji na Wafanya biashara jambo ambalo litaliongezea Shirika mapato.
Vilevile Naibu Waziri Kaspar Mmuya amelitaka Shirika hilo kuhakikisha linafunga CCtv camera kwa ajili ya kuimarisha usalama wakati litakapokuwa tayari kwa ajili ya matumizi ya kibiashara.
Hata hivyo, Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa Mkoa wa Lindi Bwn. Omary Makalamangi amemuahidi Naibu Waziri huyo kuwa kufikia tarehe Mosi Januari 2026 Mradi wa Mtanda Commercial Complex utaanza kutumika Mara moja sambamba na kuhakikisha wanapata wawekezaji wa kutosha.
Hadi Sasa Ujenzi wa Jengo hilo unatajwa kufikia asilimia 91 tangu Mchakato wake ulipoanza rasmi Mwaka 2014 ambapo kukamilika kwake kutachangia kuimarisha uchumi wa shirika na kuongeza mapato ya Mkoa wa Lindi kiujumla.